Leo Aprili 04, 2019 , Wataalam wa sekta ya ardhi kutoka halmashauri za mkoa wa Geita wamekutana kwaajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu makusanyo ya kodi ya ardhi, upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi ndani ya mkoa huu katika ukumbi wa mikutano, ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita.
Akiongea wakati wa kufungua kikaokazi hicho, Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameeleza kutoridhishwa na mwenendo wa makusanyo ya kodi ya ardhi ndani ya mkoa huku akilinganisha ukubwa wa ardhi iliyopo na ile iliyopimwa na kuona ni kama vile hakuna ardhi iliyopimwa hivyo kuwaachia wataalam hao changamoto ya kuhakikisha wanakuja na mpango kabambe wa kupima ardhi geita.
Mhandisi Gabriel amewaeleza wataalam hao kuwa, “ jamii ina changamoto, mapato ya wananchi bado ni kidogo, familia zetu bado zina changamoto, ambapo ardhi ilionekana kuipima ni gharama kubwa sana. Pamoja na serikali kutoa maelekezo na bei elekezi kwenye baadhi ya maeneo, naomba niwaache na pendekezo moja kuwa, kwanini msiwatangazie geita upimaji wa eneo kwa shilingi elfu hamsini tu ndani ya mkoa?”.
Wataalamu hao wameendelea kuelezwa kuwa, endapo wananchi watafanikiwa kupimiwa maeneo yao itapunguza kero kubwa, ardhi yao haitakuwa mfu, wataweza kupata mkopo, vitakuwa na thamani vikiuzwa lakini pia mtaepusha migogoro isiyokuwa na sababu ya watu kuingiliana mipaka.
Wito ukatolewa kwa vijana waliohitimu kwa fani ya upimaji na hawana ajira, kujitolea kuichangamkia fursa hiyo endapo pendekezo alilolitoa mhandisi Gabriel litakubalika ukizingatia tayari ofisi za kanda itaazimisha vifaa bure vya kufanyia kazi hiyo endapo vikihitajika, huku akiwataka kuhakikisha wanapangilia vizuri miji yao ili uwepo ukanda wa kijani kila unapoingia katika halmashauri husika.
Kipekee mhandisi Gabriel amekemea tabia ya watumishi wanaoendelea kusababisha migogoro ya ardhi akisisitiza utoaji wa elimu inayohusu masuala ya ardhi ili wananchi waelewe ni kwa kipindi gani watanyang’anywa eneo wasipoyaendeleza ili wawe na uelewa. Vilevile wataalam hao wamekumbushwa juu ya kupeleka kusudio la kuwashitaki wadaiwa wote ambao kwa muda mrefu sasa hawajalipa kodi za ardhi. Mkuu wa mkoa amemaliza kwa kuwasihi wataalam wa ardhi kuhakikisha wanapanga mji, na maeneo ambayo bado hayajaharibiwa ili kuwasaidia wananchi lakini vilevile kutengeneza taswira ya miji na kuifanya ikuwe.
Naye Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Charles Saguda kwaniaba ya watumishi wa sekta ya ardhi wa mkoa wa geita akamshukuru mgeni rasmi na kuahidi kuwa, ombi alilolitoa kwao watalifanyia kazi na kuleta mrejesho huku wakija na mkakati kabambe wa kuendesha zoezi zima la upimaji.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na watumishi mbalimbali akiwemo Afisa Ardhi Kanda ya Ziwa Nicolas Kawishe,Maafisa Ardhi, Maafisa Mipangomiji, Wathamini, Wapima Ardhi bila kusahau warasimu ramani
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa