Ni mwendelezo katika hatua za awali kufanikisha uanzishwaji wa vituo/masoko ya ununuzi wa madini ya dhahabu, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amekutana na kufanya mazungumzo na benki ili kuona namna zitakavyoshiriki kufanikisha jambo hili zuri na la kiuchumi.
Katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 04.02.2019 kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita na kuhudhuriwa na wawakilishi benki za BoT Kanda ya Ziwa, CRDB, NBC, NMB na Azania pamoja na ofisi ya Madini na TRA Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel amewaeleza wajumbe hao kuwa, lengo kuu ni kuanzisha soko la madini ya dhahabu haraka iwezekanavyo kwa kuzingatia uwepo wa huduma zote zinazohusiana na ufanikishaji biashara hiyo kubwa ya dhahabu.
Amesema, “nimewaita hapa lengo ikiwa ni kuona namna gani taasisi za fedha mnashiriki katika katika uanzishaji wa soko la dhahabu, nini kifanyike ili mwisho waa siku wanunuzi na wauzaji wa dhahabu wamalize mambo yote sehemu moja. Tumeamua kuondokana na hatari ya kubeba fedha nyingi, sasa twende kidijiti (digital) tukae na wateja tuwaeleze madhara ya kubeba fedha nyingi mkononi lakini vilevile tuzuie utakatishaji wa fedha”
Vile vile Mhandisi Gabriel amewapa changamoto TRA na Ofisi ya Madini Mkoa wa Geita kujipanga kuweza kuhudumia wafanya biashara wa madini na kukusanya mapato ya serikali huku utaratibu ukiandaliwa wa kuwakutanisha na kuwaelimisha juu ya namna biashara hiyo itakavyokuwa ikifanyika eneo moja kwenye kituo/soko kuu la mkoa, kisha akawatembeza wajumbe hao kwenye eneo zitakapowekwa taasisi hizo za fedha.
Wakati huo huo, Mhandisi Gabriel amependekeza uundwaji wa mfumo utakaotumika kuratibu biashara hiyo na kwamba kutakuwa na uwezo wa kujua ni kiasi gani cha dhahabu kimepatikana na kimeuzwa kwa siku, cha thamani ipi na mapato ya serikali yamekusanywa kwa kiwango gani, wazo lilipokelewa vyema na kuungwa mkono na BoT wakisema kuwa, wanaamini wataalam wao wa TEHAMA kwa kushirikiana na wa Madini, Halmashauri na TRA wataweza kufanikisha suala hilo na kwamba kama BoT wapo tayari kutoa ushauri kufanikisha jambo hilo.
Kwa upande wao taasisi za fedha wamesema, wapo tayari kuwahudumia wafanyabiashara hao wakisisitiza wananchi kutumia mifumo ya kisasa ya uhamishaji na ulipaji fedha na si kupenda kutembea na fedha taslimu kwani ni hatari kwa usalama wa maisha na wataendelea kuhamasisha suala hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa