Katika kuhakikisha kila kundi linashiriki mchakato mzima wa maboresho ya sheria mbalimbali ikiwemo za uvuvi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel Amefungua Mkutano wa Ukusanyaji Maoni ya Wadau Juu ya Sheria ya Uvuvi na ya Ukuzaji Viumbe Maji katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tarehe 01.02.2019.
Akifungua mkutano huo, Mhandisi Gabriel amewashukuru wadau wa uvuvi waliojitokeza kushiriki na kuwataka wawe sehemu ya kupinga uvuvi haramu ili kulinda rasilimali zinazopatikana kutokana na shughuli za uvuvi, huku akimpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele akisaidiwa na wizara kuipa kipaumbele na heshma Sekta ya Uvuvi.
Amesema, “nawashukuru sana wadau wa uvuvi mliofika hapa, kwakuwa zimetolewa siku thelathini, tuzitumie kutoa maoni hata kupitia tovuti ya wizara ya www.mifugouvuvi.go.tz na vituo vyote vya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kanda hii, mnakaribishwa sana. Kwetu tunaozungukwa na Ziwa Victoria ni jambo kubwa, hivyobasi tutumie vyema nafasi hii, changamoto mnazifahamu lakini pia tunahitaji kupata tija, tuboreshe sekta hii, pia kuboresha maisha yetu na nina amini baada ya mchakato huu, watalaamu wa ofisi ya mkoa wataandaa vikao na wadau ili kuja na mikakati ya kuboresha sekta hii kwa ngazi ya mkoa kwakuwa bila hivyo hatuwezi kusonga mbele”. kisha kufungua mkutano.
Akitoa madhumuni ya mkutano, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Augustine Lukanga amesema mkutano huo unatokana na shughuli za uvuvi zinazosimamiwa na kuongozwa na Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015, yenye lengo kuu kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi. Pia amesema katika kutekeleza sera hiyo ya mwaka 2015, kumekuwa na changamoto nyingi kwenye utekelezaji kutokana mabadiliko ya sayansi na teknolojia hivyo kupelekea wizara kwa kushirikiana na wadau kutoa mawazo yao na kuanza mchakato wa kukusanya maoni ili kurekebisha sheria hiyo.
Amesema, “sheria ya uvuvi ya mwaka 2003 ndiyo iliyokuwa ikisimamia maeneo makuu mawili yaani, Uvuvi lakini pia Ukuzaji Viumbe kwenye Maji ambapo baadaye ikaonekana ukuzaji viumbe kwenye maji unafanyika kwa wingi, ndyo maana imeonekana na lenyewe lipewe mamlaka yake. Hivyo kwa sasa tumeona ni vyema kuwa na sheria mbili ambazo zitasimamia maeneo hayo mawili, na leo tutapenda kusikia maoni yenu kuhusu nini kinafaa kuwa kwenye sheria hiyo kwakuwa tayari rasimu ipo, hivyo tuzipitie kuona namna zitakavyotunufaisha kiuchumi na kijamii”.
Ameeleza kuwa, uzinduzi kitaifa ulifanyika tarehe 28.01.2019 kwa kanda ya ziwa na hivyo kutolewa siku 30 kwaajili ya kutoa maoni mbalimbali, kisha kumkabidhi Mkuu wa Mkoa Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015 kama mwongozo kupanga mipango ya usimamizi bora wa rasilimali uvuvi.
Mkutano huo umehudhuliwa na kaimu Katibu Tawala Mkoa Bw. Herman Matemu, Kaimu Mkurugenzi, Ukuzaji Viumbe Maji kutoka wizarani Dkt. Hamisi Nikuli, Wataalamu wa Uvuvi wa Wizara wakiwemo Wanasheria, Maafisa Uvuvi Mkoa na Wilaya, Wenyeviti wa BMU, Wavuvi wa Dagaa, Wavuvi wa Samaki Sangara na Mazao ya Uvuvi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa