Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameendelea kufurahishwa na juhudi za wananchi wanaounga mkono kampeni aliyoianzisha ya kumaliza changamoto ya miundombinu ya Elimu na Afya ikiwemo kumaliza Zahanati kila kijiji kabla ya mwezi Juni, 2019.
Hayo yamedhihilika alipokuwa Wilayani Mbogwe kwenye ziara yake ya mkoa mzima akipita kuhamasisha shughuli za maendeleo huku akitembea kwa miguu mahali pengine kuifikia miradi iliyotekelezwa kwa jitihada za wananchi kwa lengo la kuwatia moyo. Na hapa alipita Zahanati ya Bulugala ijapokuwa haikuwa kwenye ratiba yake.
Akiongea na wananchi alipofika kujionea hatua ya ujenzi wa Zahanati ya Bulugala, Mhandisi Gabriel amesema “nawapongeza wananchi kwa namna ambavyo mmejitahidi kuanzisha ujenzi huu. Na kwa namna hii siwezi kuwaacha hivi hivi japo sikuwa na ratiba ya kupita hapa kwakuwa ni lazima kuwashika mkono wote waliohamasika na kufikisha hatua ya boma si tu kwenye Zahanati hii bali pia hata kwenye maboma ya madarasa”
Kufuatia jitihada hizo, Mhandisi Gabriel akaendesha harambee fupi iliyosindikizwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mhe. Martha Mkupasi na Mkurugenzi Bw. Elias kayandabila, bila kumsahau Diwani Nsika Sizya ambapo ilipatikana mifuko arobaini na sita (46) ya saruji, mbao kumi na mbili (12), bati Ishirini (20), na kuwaomba kufanya hesabu ya mahitaji ya bati zilizopungua ili yeye na kamati anayoiongoza waone ni kwa jinsi gani wanasaidia ukamilishaji wake.
Katika ziara hiyo , Mkuu wa Mkoa aliweza kutembelea ujenzi wa Kituo cha Afya Nhomolwa kilichopo Kijiji na Kata ya Nhomolwa ambacho hadi sasa kimegharimu kiasi cha Tshs. 98,168,500/= ikiwa Tshs. 46,194,500/= zimetoka Serikali Kuu, Tshs. 19,375,000 kutoka kwa diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Vicent Busiga na Tshs. 32,599,000/= ni nguvu za wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa aliahidi kujenga hoja kutafuta milioni mia moja kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizo akisema si kazi ndogo bali ni kubwa na yenye kustahili kuungwa mkono.
Mwisho Mkuu wa Mkoa aliongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe huku akisisitiza juu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani akiwashauri kuchangamkia fursa kwa kuandaa mradi mkakati utakaoweza kuiingizia Halmashauri mapato mengi ili iweze kujiendesha, huku akionya juu ya matumizi yasiyo sahihi ya fedha za serikali akisema ni muhimu kuzingatia miongozo ya serikali pale fedha zinapoingia.
Mkuu wa Mkoa pia akawakumbusha wana Mbogwe kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kuthibiti vifaa vya ujenzi vinapokuwa huku akiwapa mfano kuwa, tayari ofisi ya mkoa imeandaa mfumo chini ya wataalamu wa TEHAMA ambao utakuwa unaratibu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia ngazi ya msingi, ununuzi na upokeaji wa vifaa na ujenzi kwa kila hatua katika picha na taarifa ambapo hata akiwa mbali anaweza kuziona taarifa za miradi yote inayotekelezwa Mkoa mzima wa Geita lengo ikiwa ni usimamizi na uthibiti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Mhe. Martha Mkupasi akamhakikishia Mkuu wa Mkoa kuendelea kuisimamia Wilaya hiyo akihakikisha kampeni ya zahanati kila kijiji itawezekana kama ilivyo azma ya mkoa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Vicent Busiga akamhakikishia ushirikiano Mkuu wa Mkoa katika kusimamia miradi ndani ya Mbogwe huku akiomba watumishi wa Halmashauri hiyo kuwa wamoja katika kuiendeleza Halmashauri yao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Japhet Simeo akawapongeza Mbogwe kwa hatua wanayoendelea nayo katika kuahkikisha kila kata inakua na kituo cha afya na kila kijiji kinakuwa na zahanati huku akisema atahakikisha anasaidia uboreshaji wa huduma za afya mbogwe.
Kwa hakika, Geita imehamasika, vyumba vya madarasa vinajengwa, zahanati kila kijiji zajengwa na hii ni dalili kuonesha Geita inaweza kuwa ya kwanza kumaliza zahanati kila kijiji kwani ndiyo nia na lengo la mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa