Mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel amempongeza Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Flavian Kasara na kanisa la Katoliki kwa ujumla kufuatia ujenzi wa sekondari ya wasichana ijulikanayo kama Maria Malkia wa Amani Geita (Marry Queen of Peace Geita)
Ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea ujenzi wa shule hiyo oktoba 8, 2019 ambao unaendelea kwa kasi, huku majengo mengi yakiwa katika hatua mbalimbali za uezekaji, upigaji ripu na upauaji huku majengo machache yakiwa katika hatua ya boma.
“uwepo wa shule hii ni jambo jema la kuwalea watoto wa kike na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao, hata wa kwangu nitamleta hapa shule hii itakapoanza, hongereni sana. Hii shule ni yetu sote, namimi kama mkuu wa mkoa nitahakikisha mambo yote yanakwenda kwa kasi kwakuwa hakuna sababu ya kuchelewesha kuanza kwa shule hii”, alisema Mhandisi Gabriel.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa alitaka kufahamu ni jambo gani ambalo hadi sasa limepelekea shule hiyo kutokufikia hatua za usajili ili ianze kufanya kazi mwezi Januari mwaka 2020 kwa kumuita mthibiti ubora kutoka halmashauri ya mji geita Bi. Vaileth Kiiza, ambaye yeye alisema, kama wathibiti ubora wa elimu wanafurahishwa na uwekezaji huo ukizingatia kwamba serikali itanufaika kwakuwa watoto wa kike wengi watapata elimu wakiwa salama kwa kukaa bweni, hivyo kuwahakikishia viongozi wa dhehebu hilo pamoja na mkuu wa mkoa kuwa, wataendelea kutoa ushauri na taarifa kwa wakati stahiki ili kuiwezesha shule hiyo kusajiliwa kama taratibu zinavyoelekeza.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Flavian Kasara kwa upande wake amemshukuru mkuu wa mkoa kwa kufika kuwatia moyo na kuwapa ushauri mbalimbali hata wa kiujenzi huku akisema kuwa, wao wameguswa na kumlinda mtoto wa kike kwa kujenga shule hiyo kwani, wasichana wengi wamekuwa wakikatishwa elimu na wanaume wasio wema wakiwapa mimba, kitendo ambacho hata kiongozi wa Nchi Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amekuwa akikikemea kwa nguvu zote kila anapoongea na wananchi.
Askofu Kasara amekemea tabia ya wanaume wanaowadanganya mabinti kwa kuwapa vocha, huku akitoa wito kwa watoto wa kike kuishika elimu kwakuwa ina thamani kubwa kuliko vocha zinazotumika kuwadanganya wanafunzi.
Imeelezwa kuwa, endapo itakamilika, Shule ya Sekondari Maria Malkia wa Amani Geita itaweza kuchukua idadi ya wanafunzi wa kike wasiopungua mia nne themanini (480), ambapo kwa sasa, tayari imekamilisha madarasa sita, na kwa kuanza itaanza na mikondo miwili yenye wanafunzi themanini (80), yaani darasa moja wanafunzi arobaini (40) japo lengo ni kuwa na mikondo mitatu kwa kila darasa.
Shule hii ipo ndani ya eneo la jimboni mjini Geita na hadi sasa, unaendelea ujenzi wa madarasa mengine kumi na mbili (12), maktaba, bwaro la chakula na jiko lako, vyoo, chumba ya kompyuta, maabara tatu za sayansi na moja ya jiographia, mabweni mawili ye uwezo wa wanafunzi mia moja tisini na mbili (192), kila bweni likiwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi tisini na sita (96) ndani kukiwa na nyumba ndogo ya matroni pamoja jengo la utawala. Vile vile shule hii itakuwa na miundombinu ya maji, umeme na viwanja vya mpira, bila kusahau ukuta kwa ajili ya ulinzi zaidi.
Kwa hakika, endapo shule hii itakamilika, jamii itaweza kuwalinda wasichana 480 watakaotumia shule hiyo ya bweni kwa kidato cha kwanza hadi cha nne mkoani Geita.
Kwa pamoja tumlinde mtoto wa kike.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa