Ni siku ya kilele cha Wiki ya Sheria Nchini ambapo wadau wa sheria wanakutana kwa pamoja katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita tarehe 06.02.2019 na kufunguliwa kwa dua na sala kutoka kwa viongozi wa kidini.
Akihutubia wadau wa sheria mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, amepongeza juhudi zainazofanywa na mahakama katika kutoa haki na amewaonya wanaofoji nyaraka kupoteza ushahidi mahakamani na kuchelewesha haki, huku akisisitiza ushirikiano baina ya vyombo vinavyounda serikali kwakuwa iwapo kimoja hakitatoa ushirikiano, ni dhahiri utakuwepo ucheleweshwaji wa haki, vilevile akakemea rushwa.
Amesema,“nawapongeza Mahakama kwakuwa Mhe. Hakimu Kato amesema mpango ni kutokaa na kesi kwa zaidi ya mwaka. Lakini pia niwaonye mawakili kanjanja mnaopenyeza na kusababisha kukithiri kwa mikataba mibovu inayopelekea dhuruma kwa haki za wananchi. Tambueni kupitia kaulimbiu “utoaji wa haki kwa wakati ni wajibu wa mahakama na wadau”, haiwezi kufanikiwa ikiwa hakuna ushirikiano baina ya vyombo vinavyounda serikali yaani Bunge, Mahakama na Serikali” hivyo nakemea wale wote wanaovuruga ushahidi lakini wapenda rushwa kwani inapunguza uwezo wa kufikiri unashuka”.
Mhandisi Gabriel ameendelea kusema kuwa, hafurahishwi na kitendo cha mtumishi mmoja kuchafua jina la taasisi ilhali kafanya uovu kwa utashi wake mwenyewe na kuhimiza wananchi kuwa na imani na mahakama kwani ni chombo muhimu sana chapaswa kuheshimiwa.
Katika taarifa yake awali, Mhe. Jovith Kato, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita ameeleza kuwa, kama mahakama wamejitahidi kupunguza kesi, lengo ikiwa ni kutokukaa na kesi kwa zaidi ya mwaka huku akisema kwa kesi za mwaka 2018, ni nne tu ndizo bado hazijaisha na zinatarajiwa kuisha kabla ya mwezi juni huku akisema “Geita ndipo kuna matokeo makubwa sasa (Big Result Now)”.
Wakati huo huo Mhe. Kato amemweleza mkuu wa mkoa kuwa, kaulimbiu ya siku hii itatekelezwa kwa vitendo na baadaye kuwaongoza wageni waalikwa akiwemo mgeni rasmi mkuu wa mkoa kwenye mahakama kwa vitendo na kuendesha kesi mojawapo ikiwa ni ya rushwa ambapo mtuhumiwa alipatikana na hatia na kutupwa jela kwa miaka mitatu, nakala ya hukumu ikiwa imeandaliwa ikimaanisha utendaji kazi ulioboreka kwa kutoa nakala ya hukumu baada tu ya hukumu.
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Geita kupitia Wakili Bibiana Kileo amesema kuwa, si wakati wa kulaumiana kwa wadau wa sheria bali ni wa kushirikiana kutenda haki kwa wakati huku akisema “tutataifisha mali au mazao ya uharifu na hakuna atakayenufaika na vitu vilivyopatikana kwa njia isiyo halali"
Nao mawakili wa kujitekemea katika risala yao wameeleza kuwa, changamoto waliyonayo ni uwepo wa wanasheria/mawakili makanjanja wasiotambulika wanaochangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa mikataba mibovu, hivyo kuomba msaada wa serikali kudhibiti jambo hilo. Vile vile wameeleza changamoto ya mikataba kuandaliwa na viongozi wa vijiji na kata na hivyo serikali kukosa mapato na kupendekeza mikataba hiyo iandikwe na wanasheria wanaotambulika ili mteja apewe risiti ya mfumo na serikali itapata mapato yake stahiki, kisha kuipongeza serikali kwa ujenzi wa mahakama na magereza ikiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuepuka kusafiri umbali mrefu.
Elimu kwa wananchi pamoja na kuongeza juhudi kufanya kazi hata kwa masaa ya ziada ukawa ni ushauri uliotolewa kwa wadau wa sheria kwa lengo la kuongeza imani kwa wananchi, lakini wananchi pia kutoa ushirikiano ikiwemo kutoa ushahidi pale wanapohitajika na si kudanganya au kukwepa kutoa ushahidi.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Josephat Maganga, viongozi wa dini za kiislam na kikristo na watumishi wa Mahakama na wengine wa taasisi za serikali bila kusahau wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa