Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amefarijika kuona mwitikio wa wananchi wa Kijiji cha Nhwiga, Kata ya Nyamtukuza Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale katika kuhakikisha Zahanati kila Kijiji kwa Nyang’hwale inakua ni historia.
Hayo yamejiri tarehe 05.11.2018 wakati Mhe. Mhandisi Gabriel akiwa katika ziara ya kikazi mkoa mzima akianzia Wilaya ya Nyang’hwale akitembelea na kujionea hatua mbalimbali za miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ikiwemo ya elimu na afya.
Akiwa Nhwiga amesema, “nashukuru kwa mapokezi mazuri lakini pia nakupongeza mwenyekiti na wananchi wa eneo hili japokuwa mmechelewa kufanya maamuzi haya kwakuwa huu ndio msingi wa mwisho kuchimbwa hapa Nyang’hwale, lakini bado mnayo nafasi kwakuwa fedha zipo za kuleta hapa endapo mtakamilisha mapema ujenzi huu. Ningependa kuona ninyi mnakuwa wa kwanza kumaliza, na inawezekana”.
Pia Mhandisi Gabriel amewahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili ikiwezekana mapema mwezi Februari mwaka 2019 aweze kuifungua zahanati hiyo huku akisisitiza kuzingatia kanuni za ujenzi katika miradi hiyo ili iwe imara kwa kupata na ushauri wa kitaalam. Hakuishia hapo, bali pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Mariam Chaurembo kuhakikisha vijana na wanawake wa eneo hilo wanatembelewa na kupewa elimu kisha kupewa mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Mhe. Hamim Gwiyama akatumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwahamasisha wananchi hao kushiriki kikamilifu ili waweze kupata fedha za ukamilishaji ikiwa watawahi kumaliza maboma ya Zahanati hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Nyang'hwale Ndg. Adam Mtore amewapongeza wana Nhwiga huku akiwapa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kisha kuwasilisha mchango wa Chama Tawala na wa Mhe. Rais katika Zahanati hiyo akiwasisitiza kuwa Mhe.Rais anawakumbuka wana Nhwiga na hivyo ameona ni vyema kuchangia maendeleo kijijini hapo ili kusaidia utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala.
Katika kuhamasisha ujenzi wa zahanati hiyo, jumla ya mifuko hamsini ya saruji imechangwa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi (Halmashauri), Viongozi wa Wilaya hiyo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya CCM Wilaya, Ofisi ya Mbunge, Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa n.k.
Kufuatia ujio wa Mhandisi Gabriel, mwananchi mmoja alishindwa kujizuia kumuombea Mkuu wa Mkoa kwa Mwenye enzi Mungu ili ampe maisha marefu ili aendelee kuleta matokeo chanya ndani ya Mkoa wa Geita, kisha Mkuu wa Mkoa kumaliza ziara yake kwa kuwasalimia Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nhwiga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa