Na Boazi Mazigo-Geita
Zikiwa zimesalia siku 12 kufikia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martin Shigela pamoja na Katibu Tawala Mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara wameanza ziara ya kikazi kujitambulisha kwa uongozi na watumishi wa Wilaya za Mkoa wa Geita wakianzia Wilaya ya Geita Agosti 10, 2022.
Akiongea akiwa Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Geita, RC Shigela amesema, anamshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kuona kuwa yeye anaweza kumsaidia kazi kwenye Mkoa wa Geita lakini pia amemshukuru kwa fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa mkoani Geita. Vilevile, amezipongeza halmashauri za wilaya ya Geita kwa ukusanyaji wa mapato uliyovuka malengo kwa zaidi ya asilimia 100 kwa mwaka wa fedha 2021/22 huku akisisitiza mambo mbalimbali kwa watumishi wa umma.
RC.Shigela amesema, “kwakuwa mimi na RAS tumeteuliwa siku moja, tumeona ni bora leo tuambatane kwenye utambulisho na kisha baadaye kila mmoja atapata nafasi ya kuendelea na ratiba yake. Kikubwa kutoka kwenu niombe muwe wabunifu katika kuongeza mapato, wanaokusanya mapato wahakikishe fedha zinapelekwa benki kabla ya kutumiwa, mshirikiane, mpendane, mfuuate sheria, taratibu na kanuni za nchi, msimamie vyema miradi ya maendeleo, pelekeni asilimia 40 ya mapato yenu kwa wananchi, epukeni makundi, jueni yakuwa Mhe.Rais anatupenda sana na anategemea mageuzi makubwa sana kutoka kwetu”
Akimaliza, RC Shigela amesema kuwa, iko haja ya kuimarisha na kuhuisha vikao vya mashauriano ya mpango wa matumizi ya fedha zinazotokana na wajibu wa Kampuni kwa Jamii CSR kutoka Mgodi wa GGM ili Mkoa ushiriki kikamilifu lakini vilevile kuwa na mpango utakaowezesha mapema mwaka wa fedha unapoanza, mikataba iwe imesainiwa na utaratibu uanze mara moja.
Naye Katibu Tawala Mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara akiwa Geita TC na Geita DC amesema, “nimshukuru Mhe.Rais kwa kuuniteua ma kunileta Geita, hivyo basi kama watumishi tunayo kazi ya kubuni vyanzo vipya vya mapato na tuongeze ajira kwa vijana, kubwa zaidi tuchangie kwenye pato la taifa kupitia makusanyo na kodi. Yatupasa kufikia mwaka 2025 tuifikie asilimia 30 ya uuzaji mazao nje ya nchi kwakuwa hadi sasa mazao yanayoongoza ni Dhahabu na Mchele na bahati nzuri yote yanapatikana Geita, na hapo ndipo tutaipata tafsiri halisi ya kaulimbiu yetu “Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima, lengo likiwa ni kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Nao Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo, Wabunge wa Majimbo ya Geita Mhe.Kanyasu John Constantine, Mhe.Mhandisi Tumaini Magesa Pamoja na Mhe.Joseph Kasheku Musukuma wamesema, wanamshukuru Mhe.Rais kwa kuwateuwa viongozi hao RC na RAS na kwamba watwapa ushirikiano katika kuhakikisha wanafikia malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo.
RC na RAS Geita wanaendelea kujitambulisha kwenye Wilaya za Mkoa wa Geitta ambapo Agosti 11, 2022 watatembelea wilaya ya Mbogwe na Bukombe.
Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa