Na Boazi Mazigo-Geita
Ikiwa zimesalia siku 2 ili kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martin Shigela ameendelea kufurahia mafanikio yanayotokana na kazi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuinua uchumi kwa kuvutia uwekezaji kwa kuzindua duka kubwa la vifaa vya ujenzi “Dar Ceramica Centre” tawi la Geita Agosti 20, 2022, huku akitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kufanya manunuzi ya vifaa vya kisasa kwenye duka hilo na kwamba uamuzi wa mwekezaji huyo ni sahihi kwa wakati sahihi.
Akizungumza baada ya kutembelea, kukagua na kupata Maelezo juu ya vifaa mbalimbali vilivyomo kwenye duka hilo, Mhe.Shigela amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa jinsi inavyoendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba atatoa ushirikiano kwa wawekezaji wote hivyo kutumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kwakuwa halmashauri za Mkoa wa Geita zinayo meneo ya uwekezaji ikiwemo EPZA kwa halmashauri ya Mji Geita.
“niwapongeze kwa uamuzi wa kuwekeza Geita kwani ni uamuzi sahihi na kwa wakati sahihi na ni kupitia ninyi, wawekezaji wengine watakuja. Uwepo wa duka hili, utawapunguzia wanaGeita gharama za usafiri ambazo hapo awali waliziingia wakizifuata biadhaa hizi. Mzunguko wa fedha utaongezeka, hivyo niwaombe wananchi pendeni vya kwenu, njooni mnunue vifaa hapa tuboreshe makazi yetu nasi tufananie na Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima ambayo ndiyo kaulimbiu yetu kwani punguzo mmepewa la 6% kwa kila bidhaa kwa wiki nzima” amesema Mhe.Shigela.
Mhe.Shigela amemaliza kwa kuwakaribisha wawekezaji kwenye sekta za utalii, kilimo, uchimbaji madini na uvuvi na kuwasihi wananchi wote kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi kwa kutoa taarifa sahihi bila kuwaficha wenye ulemavu kisha kutangaza kuzindua rasmi duka hilo.
Akisoma taarifa ya mradi, mkuu wa kitengo cha mauzo na masoko wa Dar Ceramica Centre bw. Cosmas Patrick amesema, kampuni hiyo ilianzishwa miaka 24 iliyopita ikiwa na uzoefu mkubwa katika uuzaji wa vifaa vya kisasa vya ujenzi lakini pia inatoa ushauri wa kitaalamu juu ya matumizi ya vifaa hivyo kwa mteja na kwamba bidhaa zao ni bora na kwa gharama nafuu.
Bw. Patrick amemaliza kwa kukubali ombi la mkuu wa mkoa kutoa punguzo la bei kwa siku za mwanzo kwa kutangaza punguzo la 6% kwa kila bidhaa itakayonunuliwa dukani hapo hadi tarehe 27 Agosti, 2022 na kumpongeza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanaendelea kufanya kazi kwenye mazingira bora akisema “Dar Ceramica Centre Tumekuja Kujenga na Wewe”
Awali, katibu tawala mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara alisema anaipongeza kampuni hiyo kuchagua kuwekeza Gieta na kwamba anaendelea kushuhudia jitihada za kukuza uchumi wa nchi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita na hata kuongeza mauzo ya nje ya nchi, Geita ikiwa miongoni mwa mchangiaji mkubwa kwani dhahabu pekee ambayo kwa kiasi kikubwa hutoka Geita huchangia 40% ya mauzo ya nje ya nchi, hivyo kuendelea kuwakaribisha wawekezaji Geita.
Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa