Na Boazi Mazigo, RS -Geita
Katika kuhakikisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM inatekelezwa vyema mkoani hapa, mkuu wa mkoa Geita mhe.Martine Shigela amefanya ziara katika halmashauri ya wilaya Mbogwe na kutembelea miradi sita yenye thamani ya shilingi Bilioni Nne, Milioni Mia Saba Ishirini na Nne, Laki Tano Themanini Elfu na Ishirini na Nane (4,724,580,028) ya sekta za elimu, afya na utawala ambapo ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuwa na viongozi wenye kushirikiana hadi kupata thamani na ubora wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ikiwa katika hatua mbalimbali, huku asikisisitiza wazazi kupeleka watoto shuleni ili wapate elimu kutokana na uwepo wa miundombinu mingi ya elimu iliyojengwa.
Wito huo umetolewa kati ya Oktoba 30 na 31, 2023 wakati wa ziara hiyo iliyofanyika katika kata mbalimbali za Mbogwe ambapo RC Shigela alitembelea ujenzi wa shule mpya ya msingi ya mchepuo wa kiingereza Nyakasaluma, ujenzi wa shule mpya ya sekondari kata ya Nyakafulu, ujenzi wa shule mpya ya msingi Magufuli, ujenzi wa hospitali ya wilaya Mbogwe, ujenzi wa nyumba ya mkurugenzi pamoja na wakuu wa idara wa halmashauri hiyo ambapo ameshiriki upandaji miti katika miradi yote na kuwapongeza Mbogwe kwa utaratibu huo.
Akiongea kwa nyakati tofauti baada ya kukagua miundombinu hiyo, RC Shigela alisema, “ni vyema wazazi na wananchi kwa ujumla muone thamani ya miundombinu iliyowekwa na serikali inayoongozwa na Mhe.Rais.Dkta.Samia Suluhu Hassan na muwapeleke watoto shule, lakini viongozi hakikisheni wananchi wanafahamu kila fedha inayoletwa na serikali na juhudi ziongezeke ili kukamilisha miradi yote ili ianze kutumika. Vilevile nitoe wito kwa wazazi kuleta watoto wenu kwenye shule yetu ya mchepuo wa kiingereza ya Nkayasaluma itakapoanza kwani itakuwa ya gharama nafuu”
“wazazi msidanganyike, elimu haina mbadala, mtoto anapoenda shule ndipo atakuwa mwalimu, rais, mkurugenzi, mchimbaji, daktari n.k, hivyo muwapeleke watoto shule. Pia, naziagiza taasisi zote zinazohusika na umeme, maji na barabara kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi ili waweze kujiletea maendeleo”. Alimaliza RC Shigela kisha kushiriki zoezi la upandaji miti.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbogwe Mhe.Sakina Mohamed alianza kwa kumshukuru Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kufuatia fedha nyingi za miradi zinazoendelea kutolewa Mbogwe na kusema, “kama viongozi tumejipanga kuja na operesheni maalum kuhakikisha watoto wenye umri wa kuwa shuleni wanasoma ili tupunguze mdondoko wa wanafunzi, na niwaonye wazazi wanaowatumikisha watoto na kupelekea kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu licha ya miundombinu na shule nyingi zilizojengwa na serikali.
Naye mkurugenzi wa halmshauri hiyo Bi.Saada Mwaruka alisema, “tunamshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutujali watumishi pamoja na wananchi kwani sisi tunajengewa makazi ya kuishi, na wananchi wanaletewa miradi mingi ya sekta mbalimbali, hivyo tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kusimamia vyema fedha zote zinazoletwa".
Geita ya Samia, Hakuna Kilichosimama
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa