Ni siku moja kabla ya kikao cha ujirani mwema kitakachofanyika kuanzia tarehe 15-16.03.2019 katika mkoa mwenyeji Geita. Kipekee tena, ni siku chache kuelekea ufunguzi wa soko la dhahabu Geita utakaofanyika tarehe 17.03.2019, ambapo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe.Aggrey Mwanri ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo inawasili mkoani hapa na kupokelewa na wenyeji wao ambao ni Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita.
Baada ya mapokezi hayo, wote wanakutana na kufanya mazungumzo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na baada ya neno la ukaribisho, RC Tabora anapata nafasi ya kuzungumza.
Mhe.Mwanri Anasema, “nikushukuru sana kwa ukaribisho. Leo tumekuja kujifunza kuhusu Geita, na kwakutambua hilo, wenzangu inabidi kwanza tukiri kuwa hatujui ili tuweze kujifunza, hivyo sisi wana Tabora tuliona tuje mapema. Tuna hakika tukishajifunza, tutakuwa na badiliko la ghafla la kitabia”
Hakuishia hapo, bali Mhe. Mwanri anaendelea kugusia kuhusu elimu iliyotolewa na RC Geita wakati wa utangulizi akisema, “tumejifunza namna tunavyoweza kupata mapato ya serikali. Lakini tambueni yakuwa mkoa wenu ni wa kipekee na umebarikiwa kutoa kiongozi wa Taifa hili, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli, tunayempenda sana, anayeitetemesha dunia, hivyo tuige kutoka kwake”
Katika kikao hicho, RC Tabora anamhakikishia RC Geita kuwa, wanakwenda Tabora kutumia ujuzi watakaoupata mkoani hapa, na watakapofanikiwa watahakikisha wanaualika Mkoa wa Geita ukaone matunda ya mafundisho yake kwao, na itakuwa ni mafanikio makubwa, kwani lengo ni kupata mapato yatakayowasaidia kusukuma maendeleo mbele, huku akiendelea kumpongeza kwa kutokuwa mchoyo wa elimu kwakuwa wengine huficha siri ya mafanikio wakiogopa kupitwa kimaendeleo.
Awali akiukaribisha ujumbe huo kutoka Tabora, RC Geita Mhe.Mhandisi.Robert Gabriel ametumia ubao kufafanua mambo mbali mbali akiwaambia wajumbe hao kuwa, “siri kubwa ya ya mafanikio ni kuishirikisha jamii, usimamizi mzuri, kuwa na uongozi bora, bila kusahau maadili na mtandao mwema”
Mhandisi Gabriel amewaeleza pia juu ya namna alivyosimamia fedha zitokanazo na migodi, yani fedha za wajibu wa makampuni kwa jamii (CSR), ambapo kupitia mgodi mmoja wa dhahabu Geita (GGM), miradi mbalimbali imetekelezwa ikiwemo ya elimu na afya pamoja na ile ya kimkakati kama vile vibanda vya soko, uwekaji taa barabarani, pamoja na uandaaji wa eneo la kipekee la uwekezaji, ukanda wa utalii bila kusahau maeneo ya maonesho.
Baada ya kumaliza mazungumzo ofisini, Mhandisi Gabriel anaupeleka ujumbe wa Tabora kushuhudia baadhi ya miradi inayotekelezwa na fedha za CSR ikiwemo vibanda kuzunguka soko kuu, ndani ya Halmashauri ya Mji Geita. Hakika wamejionea na kujifunza mengi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa