Na Abraham Mwasimali- RS Geita
Katika kuendeleza jitihada za kuimarisha afya ya uzazi wa mama na mtoto, mganga mkuu Mkoa wa Geita Dkt.Omari Sukari alitoa wito kwa wadau kujadili usalama na namna ya upatikanaji wa bidhaa za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Wito huo ulitolewa Novemba 1, 2023 wakati akifungua kikao kazi kujadili masuala yahusuyo afya ya uzazi wa mama na mtoto kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa hoteli ya Alphendo iliyopo mjini Geita.
Akifungua kikao kazi hicho, Dkt.Sukari alisema lengo ni kujadili namna ya kuweka mipango madhubuti ya upatikanaji wa bidhaa za afya ya uzazi, mama na mtoto ili zinapatikane muda wote kwa ajili ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga lakini pia bidhaa hizo zitawasidia vijana wa rika balehe ambao pia ni wanufaika wa huduma hizo.
‘’tutajadili hasa namna ya upatikanaji wa bidhaa za afya muda wote kwa ajili ya wakina mama wanao toka kujifungua ili kupunguza hali ya vifo kwa watoto wachanga na wajawazito vinavyojitokeza na pia wanufaika wengine ni vijana wetu ambao wapo kwenye rika la kubalehe ambao pia ni wanufaika wa afya ya uzazi kwa vijana’’. Alisema Dkt Sukari
Aidha katika hatua nyingine, Dkt Sukari alisema lengo jingine ni namna ya kuwafikia wananchi kwa ajili ya kujua umuhimu wa matumizi ya uzazi wa mpango kwa njia ya kisasa ili kupunguza vifo vya watoto wachanga pamoja na vifo vya mama wajawazito.
“kwa mujibu wa tafiti ya “Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator” (TDHS-MI), asilimia 22 ya kina mama kati ya umri wa miaka 15 mpaka 49 wanatumia njia za uzazi wa mpango. Hii bado ni asilimia ndogo, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunafikia asilimia 45 za kutumia matumizi ya kisasa ya uzazi wa mpango kama lilivyo lengo la Taifa. Hali ya vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 556 mpaka 104 kwa vizazi hai 100,000 kwa Taifa, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha dawa za dharura zinakuwepo ili kuendelea kupunguza vifo hivyo’’. Aliongeza Dkt.Sukari
Kwa upande wake mjumbe wa kikao hicho bw. Hemedi Mahamudu alisema kuwa, kamati ya kikao hicho itahakikisha kinatoa njia madhubuti katika kuhakikisha huduma za afya ya uzazi wa mama na mtoto zinatolewa kwa wakati wote kwa kuzingatia uwepo wa dawa muhimu kwa kila kituo cha afya, pamoja na kuzisimamia dawa ili ziweze kuwafikia walengwa wa huduma hii ili kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto.
‘’ndugu wajumbe wa kikao hiki, tunatakiwa tuweze kuimarisha njia mahususi za upatikanaji wa bidhaa za afya ya uzazi wa mama wajawazito na watoto ili tuweze kupunguza kiwango cha vifo vya kina mama wanaotoka kujifungua, watoto pamoja na vijana walio katika kipindi cha barehe Pia, ni vyema tuhakikishe tunatoa dawa kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kwa mujibu wa takwimu za wagonjwa tulio nao”. Alimaliza bw. Mahamudu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa