Na Boazi Mazigo-Geita
Mkuu wa Mkoa Geita Mhe. Martin Shigella amesema kwa sasa pamoja na shughuli zinazoendelea, kipaumbele cha Serikali ni zoezi linalokuja la Sensa ya Watu na Makazi.
Amesema hayo Agosti 5, 2022 akiwa ofisini kwake punde tu baada ya kulakiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wa Chama Tawala CCM pamoja na Sekretarieti ya Mkoa na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita.
Akiongea baada ya kupokelewa RC Shigella ameeleza yakuwa, amefarijika kuwa mkoani Geita na anamshukuru Mhe.Rais kwa kumuamini na kumteua kuwatumikia Watanzania wa Geita huku akisema “ninamshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na niwashukuru kwa ukarimu wenu wakati wa mapokezi na niwapongeze kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kikubwa tushirikiane kuendeleza mazuri ambayo wenzetu waliyafikia na kuboresha zaidi palipo na changamoto”.
Aidha, RC Shigella ameeleza kuwa, “kipaumbele chetu ni kuwatumikia wananchi, tukatatue kero zao, tuwafuate walipo na tusisubiri watufuate maofisini. Tutambue Mhe.Rais ana matarajio mengi na wananchi wanamuamini, hivyo tusimwangushe. Lakini pia pamoja na kazi nyingine, Sensa ya Watu na Makazi ni kipaumbele chetu kwa sasa hadi Agosti 23, hivyo viongozi wote tuhakikishe tunashiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi washiriki na tupate taarifa sahihi tuweze kuisaidia serikali kupanga vyema kwa ajili ya maendeleo”.
Mhe.Shigella amemaliza kwa kuhimiza ushirikano miongoni mwa watendaji, wananchi na wadau mbalimbali na kuwakumbusha watendaji kuhakikisha wanaweka juhudi na kuboresha mikakati katika ukusanyaji wa mapato huku akizipongeza Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2020/21 na kuipongeza Serikali kwa kuleta fedha nyingi za bajeti zikiongezeka mfululizo kwa miaka mitatu kutoka zaidi ya Bilioni 222.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23 hadi zaidi ya Bilioni 288.4 kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Mkoa wa Geita ulipata viongozi wapya baada ya uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan Julai 28, 2022 ambapo Mhe.Martin Reuben Shigella aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Geita na Prof.Godius Walter Kahyarara aliteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa Geita na tayari wamewasili mkoani hapa na kuanza kazi wakati zoezi la makabidhiano lilingojewa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa