Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajali na kuvithamini vyama vyote vya Ushirika Nchini kwa sababu ni mojawapo ya msingi wa maendeleo ya Taifa.
Mhe. Shigela ametoa kauli hiyo alipokuwa akiongea na wanachama wa vyama vya Ushirika kutoka katika Wilaya zote za Mkoa wa Geita wakati wa Maadhimisho ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika katika Mkoa wa Geita ambalo limefanyika Mei 16, 2025 katika Ukumbi wa CCM Wilayani Bukombe.
Mhe. Shigela ameeleza kuwa Serikali kupitia wataalam wake imeendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa vyama vya ushirika kwa wanachama mbalimbali, pia iliona changamoto zinazowakabili wana ushirika katika utendaji kazi zao za kila siku ikaanzisha Taasisi ya kifedha kwa ajili ya kuwawezesha wanachama hao kupata mikopo yenye riba nafuu.
“Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshalifanyia kazi suala la mikopo na upatikanaji wa mikopo kupitia Benki ya Ushirika Tanzania, Pia wakulima na wafugaji wameendelea kunufaika na mbegu bora za mazao, madawa ya mifugo pamoja na pembejeo zote za kilimo na mifugo hivyo ndugu zangu wana ushirika hatuna budi kutoa shukrani zetu za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwezesha.” Aliongeza Mhe. Shigela
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Geita ametoa agizo kwa watumishi pamoja na makampuni ambayo yana madeni katika vyama mbalimbali vya ushirika kulipa madeni hayo ili kuwezesha vyama hivyo kuendesha shughuli zao bila mikwamo.
Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Geita Bi. Doreen Mwanri amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na baadhi ya vyama vya ushirika kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati na hivyo kuweka malimbikizo ya madeni ambayo huzorotesha maendeleo ya sekta ya Ushirika pamoja na baadhi ya Makampuni ya ununuzi wa mazao ya kilimo kushindwa kulipa ushuru/ tozo mbalimbali kwa vyama vya Ushirika na kusababisha makusanyo ya Serikali kuwa hafifu na kutofikiwa malengo yaliyopangwa.
Mkoa wa Geita una jumla ya Vyama vya Ushirika 600, ambapo vyama 298 vimesajiliwa kwenye mfumo wa MUVU vikiwa na wanachama 25,249. Vyama hivi vimegawanyika katika Sekta mbalimbali za uzalishaji kama vile Kilimo, mifugo, uvuvi, SACCOS na jamii. Maadhimisho ya Jukwaa la Ushirika mwaka 2025 lililongozwa na Kauli Mbiu isemayo “USHIRIKA HUJENGA ULIMWENGU ULIO BORA.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa