Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kujenga mazingira rafiki katika kuwawezesha wachimbaji wadogo mikopo na mitambo ya uchimbaji katika makundi mbalimbali wanayoyaunda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa kauli hiyo hivi karibuni mjini Geita alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza kwa wingi kwenye hafla ya ufungaji rasmi wa Maonesho ya saba ya Teknolojia ya Madini iliyofanyika katika viwanja vya EPZ Bombambili Geita mjini.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa wachimbaji wadogo wamechangia asilimia 40 katika sekta ya madini kutoka asilimia 10 hivyo makundi ya mbalimbali kama kundi la wanawake na vijana watapatiwa mashine za kuchorongea ili waweze kuchimba kisasa na uhakika tofauti na uchimbaji wa kubahatisha.
“Napenda kutoa wito kwa wachimbaji wote wa madini kuacha tabia ya utoroshaji wa madini au biashara zisizo halali badala yake pelekeni dhahabu zenu na aina nyingine za madini katika masoko maalum yaliyotengwa na Serikali maalum kwa shughuli ya uuzaji na ununuzi wa madini ili muweze kuuza madini hayo kwa bei elekezi na kusaidia kukuza uchumi wa Nchi.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Umoja wa wachimbaji wadogo (FEMATA) kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo Nchini na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameeleza kuwa jumla ya wachimbaji wadogo 3,301 wamepatiwa leseni ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake mkoani humo Oktoba 2022.
Mhe. Shigela ameongeza kuwa uchumi wa Mkoa wa Geita unategemea hasa wachimbaji wadogo ambao kwa mwaka 2023 walizalisha kilo za Dhahabu Zaidi ya elfu 16 zenye thamani ya shilingi trilioni mbili. Pia ameeleza mipango ya uboreshwaji wa uwanja wa Maonesho EPZ Bombambili kuwa wa kisasa kwa kujenga majengo ya kudumu na kupewa hadhi ya kuitwa uwanja wa Maonesho wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa