Naibu Waziri wa Afya anayeshughulikia masuala ya Maendelo na Ustawi wa Jamii Mhe. Mwanaidi Khamis amesema Serikali itawasomesha watoto watatu walionusurika kwenye kadhia ya mama yao kuwapa Sumu hadi watakapoanza kujitegemea.
Mhe. Khamis amesema hayo leo desemba 07, 2021 alipofanya ziara Mkoani Geita mahsusi kwa masuala ya maendeleo na Ustawi wa jamii hasa kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya ustawi wa Jamii kufuatia tukio la hivi karibini la mama kunywa na kuwanyweshwa Sumu watoto 5 Wilayani Chato ambapo watoto wawili walifariki na watatu wamepatiwa matibabu na kunusurika.
"Kwa serikali ni msiba mzito na kwetu kama wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii tumesikitishwa sana na ndio maana tumeona tufike kutoa elimu ili wengine wasipate kadhia kama hizo tena." Amesema Mhe. Mwananidi.
Vilevile, Mhe. Naibu Waziri amewaasa wananchi kutokaa kimya na msongo wa mawazo wakifikwa na jambo hadi kufikia kufanya kitendo kama hicho bali waonane na uongozi wa vijiji na kata zao kwa ajili ya kuomba msaada.
"Niwaagize Maafisa Ustawi wa Jamii na Viongozi wa Vijiji wajipange katika ratiba zao za kazi ili kuangalia matatizo ya wananchi na kutoa elimu, wananchi wanakosa elimu kwenye masuala mbalimbali ya kijinsia, kutokana na Elimu kuwa ndogo ndio maana yanatokea mambo kama haya." Amesisitiza Mhe. Mwanaidi.
Aidha, Mhe. Naibu waziri amezungumzia fedha za mapato ya ndani 10% kukopeshwa kwa makundi maalum ya kisheria ili wananchi waondokane na changamoto mbalimbali za kimaisha huku akibainisha kuwa mama huyo asingefikia hatua ya kunywa sumu kama angekua kwenye hali nzuri ya maisha.
Amesema watoto manusura wa tukio hilo wawepo kwenye vituo vya kulea watoto yatima na mwezi Januari waunganishwe kwenye mfumo rasimi wa elimu na Serikali ipo bega kwa bega na watapata elimu mpaka watakapojitegemea.
Wakati huo huo, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule amewaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuendelea kutoa Elimu ya Maisha kwenye jamii katika ngazi zote ili hali kama hiyo isitokee tena na amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu watoto waliokosa Elimu kwa sababu mbalimbali kurudi shuleni huku akitolea mfano wa watoto manusura wa tukio la kunyweshwa sumu kuwa sasa wataunganishwa kwenye Mfumo rasmi wa Elimu.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Geita, Ndugu Frank Moshi amesema Idara ya Afya Mkoa wa Geita imefuatilia kwa karibu kadhia hiyo na tayari wameshawafikisha watoto manusura kwenye Makao ya kulelea watoto na kwamba wataendeela kuwafuatilia kwa karibu kwenye malezi na makuzi ili wawe na afya njema kwa Ustawi wa Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa