Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Dkt.Hussein Mwinyi amepongeza utendaji wa kampuni ya ya Ujenzi ya SUMA JKT Construction Ltd iliyo chini ya Jeshi ya Kujenga Taifa kwa namna ambavyo kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali hapa nchini kwa kuzingatia thamani ya fedha, viwango na ubora.
Amesema hayo Agosti 29, 2019, wakati akihitimisha ziara yake Mkoani Geita kwa kutembelea miradi inayotekelezwa na Kampuni hiyo ya ujenzi inayotekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali kwa Washitiri (wanunuzi) wake wa Kanda ya Ziwa wa SIDO, CWT, Halmashauri ya Wilaya Chato, TANAPA Pamoja na TARURA Chato huku akitaja lengo la ziara hiyo ni kutembelea miradi inayotekelezwa na SUMA JKT ili kujionea mwenyewe changamoto na mafanikio na kama kuna changamoto wao kama JKT waitatue.
“niwashukuru serikali ya mkoa wa Geita kuanzia mkuu wa mkoa Mhandisi Robert Gabriel na serikali ya wilaya kwa mapokezi mazuri, vilevile naipongeza Kampuni ya Suma JKT, ninafarijika wanajenga vizuri, kwa Kiwango na Kwa kuzingatia muda na thamani ya fedha, lakini kubwa zaidi karibu washitiri wake wengi wameisifu kampuni hii kwa kazi nzuri inayoifanya lakini kwa yale mapungufu yanayojitokeza yatarekebishwa na ni imani yangu yatarekebishwa” alisema Waziri Mwinyi.
Waziri Mwinyi ameendelea kusisitiza kuwa, kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT kwa upande wake inaendelea vizuri, kwani kazi zilizosimma ni kutokana na washitiri wake kushindwa kutoa fedha kwa wakati, hivyo kutoa wito kwa washitiri kutoa fedha kwa wakati ili kukamilisha kazi wanazopewa.
Kipekee waziri huyo akatumia fursa hiyo kufikisha ujumbe kwa vijana na taifa kwa ujumla kufahamu kuwa, nia na dhumuni la JKT ni kuwapa vijana mafunzo ya kizalendo, stadi za maisha, kuwapa mafunzo ya kijeshi ili wawe tayari kutumikia jeshi la akiba, hivyo si vyema kulalamikwa kuwa JKT haijawaajili, wajue hawapelekwi mafunzo ili waajiriwe wote, ila nafasi inaporuhusu wanaajiriwa akitoa mfano kuwa kwa mwaka wanaajiriwa vijana elfu ishirini (20,000).
Pia Waziri Mwinyi amesema, JTK inayo kampuni ya Ulinzi ya SUMA Guard ambapo wadau mbalimbali wanaalikwa kutumia walinzi kutoka kampuni hiyo ili kupunguza vijana wengi waliokosa ajira kama ambavyo Wilayani Bunda walivyofanya kwa kuchukua vijana 400.
Katika hatua nyingine, Kaimu Meneja Ujenzi wa Kanda ya ziwa kutoka SUMA JKT Kapteni Fabian Buberwa amesema, kusimama kwa ujenzi wa Ofisi ya CWT ya Mkoa ni kutokana na mshitiri huyo kuchelewesha fedha hivyo endapo zitawahishwa, kazi hiyo itakamilika mapema.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa CWT Mkoa wa Geita ndg. Kuyobya Victor, amesema anaamini jengo hilo ambalo lipo hatua ya ukamilishwaji litakamilika mapema mwezi desemba 2019 hadi Januari 2019 kutokana na changamoto walizozipata hivyo kupelekea kukwama kwa ukamilishwaji wa miradi yake.
Wakati Waziri Mwinyi akiwa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Mganga Mkuu Wilaya Dkt. Benedicto Ngaizo alimweleza na kuwa, anaishukuru kampuni ya SUMA JKT kwa ujenzi iliyoufanya ya Ujenzi wa Vyumba vikubwa viwili vya Upasuaji na kimoja kidogo huku akizitaja baadhi ya changamoto zinazohitaji marekebisho ili mradi huo ukabidhiwe japo umeshaanza kufanya kazi kutokana na ombi la barua kutoka kwa Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya Chato la hitaji la kutumika kwa huduma hiyo, jengo linalofadhiliwa na Fedha kutoka Mgodi wa Dhahabu Geita GGML Shilingi Milioni Mia Nne Kumi na Mbili (Tshs.412,000,000/=)
Aidha, Dkt.Mwinyi pia alifika na kutembelea maendeleo ya barabara iliyokamilika ya Km.2, ujenzi wa maghala/vibanda vya wajasiriamali vinne kwa gharama ya Milioni 257 kila kimoja pamoja na ofisi moja ya gharama ya shilingi milioni 260 za SIDO Wilayani Chato kisha akamalizia ziara Yake katika eneo itakapojengwa Hoteli ya Kitalii ya Nyota Tatu ya Burigi-Chato inayokadiriwa Kughalimu Kuanzia shilingi bilioni tatu na Kuendelea ambapo kwa sasa mradi huo upo katika hatua ya kukusanya vifaa vya kazi (mobilization), ujenzi wa Nyumba ya site ambapo kwa sasa tupo hatua ya kusaini makubaliano (MoU) kisha kusubiri michoro ya majengo na ujenzi, ili waanze ujenzi ingawa hatua walizofikia pia wameshauriwa na mhandisi mshauri Chuo cha Ardhi.
Tayari ziara kutembelea miradi inayotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT kanda ya ziwa imefanyika kwenye mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu na Geita kisha Shinyanga itafuata.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa