Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeguswa kwa namna ambavyo mkoa wa Geita umejidhatiti katika usimamizi mapato yatokanayo na madini sanjari na usimamizi wa mchango wa migodi kwa maendeleo ya jamii.
Taarifa hiyo imetolewa jana na Waziri wa Madini nchini Angellah Kairuki aliyekuwa ziarani mkoani hapa akiwa ameambatana na ujumbe wa DRC ulioongozwa na Waziri wa madini wa nchi hiyo Martin Kabwelulu.
Katika hotuba yake kwa wanahabari,waziri Kairuki alisema,Kongo imefurahishwa na hatua ya mkoa wa Geita kwenye usimamizi mapato ya madini pia mchango wa migodi kwa maendeleo ya wananchi wanaozunguka maeneo hayo ya migodi.
Aidha waziri Kairuki alisema,makubaliano kadhaa yamefikiwa kati ya Tanzania na DRC kuhusiana na sekta hiyo ya madini hatua ambayo inalenga kuleta tija zaidi mataifa husika na pia wananchi wa pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki,ziara hiyo ya waziri wa madini wa DRC inalenga kubadilishana uzoefu na utaalam katika uendelezaji na usimamizi sekta ya madini sanjari na kuimarisha uhusiano Tanzania na nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Alisema,ujio wa ujumbe huo pia utasaidia kubadilishana uzoefu kuhusiana na mabadiliko ya sheria za madini yaliyofanywa kati ya nchi hizo mbili huku yakiwepo makubaliano ya kuboresha mahusiano ya kimkakati ambapo Kongo imeahidi kuiunga mkono Tanzania kwa masula ya mashtaka dhidi ya makampuni ya uwekezaji.
Pia kuna suala la makubaliano juu ya kuendelea kuboresha mifumo ya udhibiti utoroshwaji wa madini yanayotoka nchi ya Jamhuri ya kidomokrasia ya Kongo na Tanzania kwa manufaa ya pande hizo mbili.
Waziri Kairuki aliongeza kusema kuwa,wageni hao kutoka DRC wapo nchini kwa ziara ya siku nne na tayari wamekutana na menejimenti ya wizara ya madini na taasisi zake wakibadilishana uzoefu namna wanavyosimamia sekta ya madini ikiwemo shughuli za uchimbaji mdogo wa madini.
Waziri Kairuki alisema,hayo yote yanalenga kuhakikisha rasilimali madini zinanufaisha zaidi mataifa haya mawili huku fursa za biashara na uwekezaji kupitia sekta ya madini pia zikiweza kuangaliwa kwa mapana yake.
Waziri Kairuki pia alisema,nchi ya DRC kwenye sekta ya madini inazalisha asilimia 70% ya madini ya Colbat inayozslishwa Duniani huku wakikabiliwa na changamoto ya kuisafirisha ikiwa ghafi na pia hawana umeme wa kutisha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Kutokana na hali hiyo,waziri Kairuki alisema kwa vile Tanzania imeanza kujidhatiti kwa kuwa na vinu vya uchenjuaji na uyeyushaji madini mazungumzo yanaendelea ili DRC kuja kufanya uchenjuaji na uyeyushaji hapa nchini.
Katika ziara hiyo ya waziri Kairuki amesema,amewakaribisha wageni wake hao kutumia bandari zetu katika kusafirisha madini yao pamoja na kuwa na majukwaa mahususi ya madini 'Mining Forum kati ya nchi za Tanzania na ile ya DRC.
Wageni hao wa Waziri wa Madini Anjellah Kairuki walipata fursa ya kutembelea mikoa ya Shinyanga na Geita ambapo Shinyanga mgodi wa Williamson Diamonds Ltd na mgodi wa wachimbaji wazawa Busolwa Gold mine na Nsangano Gold mine waliweza kutembelewa.
Kwa upande wake Mhe. Martin Kabwelulu Waziri wa Madini wa Congo ameshukuru sana kwa namna alivyopokelewa na Mhe. Kairuki na kusema hakika Tanzania na Kongo ni ndugu. Pia amesema Kongo watakuwa tayari kusaidiana na Tanzania hata pale zitakapotokea kesi zinazopelekwa kwenye mahakama ya usuluhishi kutokana na mabadiliko yaliyofanyika kwenye sheria ya madini kwa mustakabali wa nchi. Pia Waziri Kabwelulu amesema Alhamisi ya wiki ijayo atautuma ujumbe mkubwa kutoka Kongo DRC ili waje kujifunza Tanzania kwa uelewa zaidi.
Naye Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita hakusita kuupigia debe Mkoa wa Geita ili endapo mipango itakamilika viwanda hivyo vijengwe Geita kwakuwa ni jirani na Kongo na inayo madini na uzoefu wa kufanya kazi ya uchenjuaji na uchakataji wa dhahabu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa