Ni Juni 24, 2019 ambapo jumla ya kaya Sabini na Nne (74) za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) kutoka kijiji cha Nyambaya, Kata ya Katoma, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Wilaya na Mkoa wa Geita wameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na namna wanavyoendelea kunufaika na mpango huo, huku wakitoa shuhuda za mafanikio waliyoyapata kutokana na kutumia fedha wanazozipata ipasavyo.
Pongezi hizo zimetolewa kwa serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alipowatembelea walengwa hao katika ziara yake ya kikazi, ambapo amewapongeza kwa namna walivyoanzisha miradi mbalimbali ili kujikwamua na umasikini lakini pia kwa kujiunga na bima ya afya, huku akiwaahidi kufikisha salamu na shukrani hizo za pongezi kwa Mhe. Rais.
“niwapongeze viongozi kuanzia ngazi ya kijiji hadi halmashauri kwa usimamizi mzuri, nimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuendelea kuwajali wananchi. Niwaombe wafugaji na wakulima muendelee msikate tama, wataalam watakuja kuwapa mafunzo zaidi mpige hatua, lakini vile vile niwapongeze kwa kuwa na hisa kwa kuweka na kukopa, huu ni mwendelezo mzuri ni vyema msichoke na msitumie fedha hizi kulewa na kuoa oa”, alisema Mhandisi Gabriel.
Mhandisi Gabriel ametembelea baadhi ya kaya ikiwemo ya Bi. Lucia Matome na mumewe Mzee Laurent Manyanya wa umri wa Miaka sabini na nne (74) kushuhudia ni kwa jinsi gani walengwa hao wameweza kubadilisha maisha yao kwa fedha wanazozipata na kuwatia moyo kuwa wasiogope kuchekwa, bali waendelee kuchapa kazi baada ya kuona shamba wanalolimiliki lenye ukubwa wa ekari nne (4) likiwa na migomba, nanasi pamoja na mihogo.
Bi. Martha Edward, Bi. Ester Constantine na Bi. Rhoda Nicodem ni baadhi ya walengwa wa mpango huu kutoka Nyambaya nao wameeleza kuwa, kupitia TASAF III wamewaweza kujenga nyumba wakiezeka kwa bati, kuwa na mifugo kama Kuku, Mbuzi na Ng’ombe, kununua mashamba na kukodi mashamba. Bi Martha kwa upande wake anamiliki nyumba mbili (2) za bati, mbuzi watatu (3), ng’ombe wawili (2) pamoja na kilimo cha biashara bila kusahau kusomesha watoto.
Kwa hakika shuhuda zilizotolewa na kuonekana, zimedhihirisha kazi kubwa inayofanywa na TASAF, jambo linalowafanya viongozi wa Nyambaya akiwemo Bw. Musa Kisena (mtendaji wa kijiji cha Nyambaya) na wa Halmashauri akiwemo Bw. January Bikuba ambaye ni kaimu mkurugenzi mtendaji na waratibu wa TASAF ngazi ya wilaya na mkoa kuona ipo haja ya kuongeza jitihada ya mafunzo ili kuwainua zaidi kiuchumi walengwa hao.
Awali katika taarifa ya mtendaji wa kijiji ilionesha kuwa, mpango huo ulianza mwezi julai, 2015 na hadi hivi sasa ni awamu ya ishirini na mbili (22) kwa walengwa sabini na nne (74) kupokea fedha na wote wamejiunga kwenye bima ya afya, lakini vilevile kuwa na mfuko wa kukopeshana kwa riba ya asilimia kumi (10%) na kurejesha kila mwisho wa mwezi, ikiwa walianza na hisa za zaidi ya sh. laki moja ishirini na nne (TShs.124,000/=) na hivi sasa kuwa na jumla ya sh. milioni moja na laki sita (Tshs.1,600,000/=).
Kweli TASAF ni Maendeleo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa