Yawezekana wengi wetu hatufahamu ni kwa jinsi gani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawakumbuka wananchi wake kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayoitekeleza TASAF ikiwemo.
Kutana na ushuhuda mfupi wa bibi Malosha Shingisha (100), mkazi wa kijiji cha Ibambila, Kata ya Nyang’hwale, Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita ambaye ni Mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) alipotembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Juni 25,2019 katika ziara yake kufuatilia maendeleo ya walengwa wa TASAF ndani ya Mkoa huu.
Bibi Malosha anaeleza kuwa, yeye ni miongoni mwa walengwa wanaotoka kwenye kaya masikini na kwamba awali hakuweza kumudu gharama za maisha ikiwemo kushindwa kupata mlo zaidi ya mmoja kutokana na ugumu wa maisha aliyokuwa nao ukilinganisha na sasa.
“naishukuru sana serikali yetu inayoongozwa na Rais Magufuli kupitia mpango huu wa TASAF kwani umeniwezesha sana. Sasa nimejenga nyumba, nimenunua kuku ninafuga, mbuzi saba na kondoo mmoja lakini nasomesha wajukuu watatu na ninalima. Namshukuru sana Rais Magufuli kwa kuendelea kuruhusu fedha hizi kutufikia. Zimebadilisha maisha yangu na familia yangu”,asema bibi Malosha.
Kwa upande wake mhandisi Gabriel ameendelea kushuhudia mabadiliko kwa wananchi wa Geita Walengwa wa Mpango wa TASAF huku akiwapongeza viongozi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, halmashauri na mkoa kwa namna wanavyosimamia vyema mpango huo, vilevile kuwataka wataalam kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali ili kuwaimarisha zaidi huku akiishukuru serikali ya awamu ya tano kwa jinsi inavyoendelea kuwajali wananchi wake.
Taarifa iliyotolewa na mtendaji wa kijiji hicho bw. Charles Nhungukila inaeleza uwepo wa mpango huo tangu mwaka 2015 una walengwa/kaya 96 ambazo awali zilimudu kupata mlo mmoja kwa siku lakini sasa hupata milo mitatu kwa siku, maisha yao yamebadilika.
Shughuli wanazojishughulisha nazo haswa ni kilimo, ufugaji, uuzaji maziwa, wamejenga nyumba, wanamiliki na kukodi mashamba n.k
Kupitia bibi huyu, jamii inapaswa kuelewa kuwa, mtu haitaji kuwa na fedha nyingi ili kupiga hatua kimaendeleo kwani walengwa wengi hupokea fedha hadi shilingi elfu ishirini kila baada ya mwezi mmoja na huitumia vizuri hadi kuwaletea mabadiliko. Wengi huanza kwa kufuga kuku, kisha zinapoongezeka hubadilisha kwa mbuzi, kisha ng’ombe na kuwawezesha kumiliki ardhi na kujenga pia.
Hivyo basi kwa ushuhuda huu, kila aliyebarikiwa kuwa na nguvu anapaswa kujishughulisha apate kipato ili kuepukana na jamii tegemezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa