Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekutana na viongozi wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa na kutoa semina juu ya Huduma za Utangazaji kwa Maudhui yanayotazamwa Bila Kulipiwa (FTA) tarehe 08.10.2018 katika Ukumbi wa Mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa, TCRA ni taasisi muhimu sana kwakuwa inalo kujumu la kusimamia sekta ya mawasiliano ya utangazaji, inayohitaji umakini sana wakati wote kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwa kuhakikisha huduma za utangazaji zinawafikia wananchi wote, kuwa na miundombinu bora na endelevu na maudhui yanayotangazwa na vituo vyetu yaendelee kuleta Amani, Mshikamano na Umoja wa Taifa letu.
Amesema, “leo ni siku nzuri ya kupata elimu inayogusa kwa upana huduma za utangazaji zinazotolewa hapa nchini, na ni vyema tukawa wanafunzi bora ili tuweze kuelewa masuala mengi yanayohusu sekta hii kwa kuwa sisi sote ni wadau”. Kisha akamaliza kutoa neon la ufunguzi kwa kusema ni matarajio yake kuwa, semina hiyo itatoa ulewa mpana na kufanya mjadala kupitia maswali mbalimbali na kutoa wito wa kuwa mabalozi wazuri wa TCRA kufuata masharti ya Chaneli (maudhui) zinazotazamwa bila malipo kwenye visimbuzi vya Azam, DSTV na ZUKU.
Naye Mhandisi wa Mawasiliano kutoka Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Francis Mihayo akatoa semina kwa viongozi wa MKoa akianza kwa kutoa historia ya mabadiliko kuwa, awali mfumo uliokuwa unatumika katika urushaji wa matangazo ulikuwa Analojia na sasa tumehamia Dijiti (digital).
Na mfumo huo wa analojia ulikuwa umegawanyika katika makundi mawili
1. Mtoa huduma, aliyekuwa na jukumu la kuandaa maudhui
2. Kujenga miundombinu ya kurushia maudhui
Baada ya Teknolojia kubadilika, yakaja makundi mawili ambayo ni
1. Wanaoandaa Maudhui pekee
2. Wanaorusha Maudhui pekee
Hali hii ndiyo iliibua visimbuzi (Ving’amuzi) vinavyopewa leseni na TCRA ambapo wote waliopata leseni kwa ajili ya kubeba chaneli zilizokuwepo kabla ya kuingia kwenye mfumo wa Dijiti (digital) ni kampuni tatu ambazo ni
1. Basic Transmission Ltd lenye visimbuzi vya Digitek na Continental
2. Star Media lenye kisimbuzi cha Star Times
3. Agape Associate lenye kisimbuzi cha Ting
Hivyo basi hayo ndiyo makampuni yenye dhamana kwa mujibu wa sheria kubeba chanel ambazo zilikuwepo kabla ya kuhamia mfumo wa Dijiti.
Yapo pia makampuni matatu yaliyopewa leseni na TCRA yaliyopewa leseni ya kurusha matangazo kwa ajili ya kulipia (Content by Subscription) lakini vilevile kwa mujibu wa Makubaliano ya Shirika la Mawasiliano duniani kubeba chaneli ya Taifa kwenye kila nchi husika ambayo ni
1. Azam Media
2. Zuku
3. DSTV
Akaongeza kwa kusema sifa za kuwa na maudhui yasiyolipiwa zikiwemo
1. Kutoa Taarifa ya habari (Kuhabarisha jamii inayoizunguka)
2. Kutoa Habari za watoto (kutenga masaa 2 kwa wiki kwa kipindi cha watoto)
3. Kutoa mijadala inayohusu wananchi wanaowazunguka kitaifa kwa maendeleo ya nchi
4. Maagizo na maelekezo ya viongozi mbalimbali
Kwa upande wa waandaa maudhui ya kulipia wana sifa zifuatazo
1. Kurusha tamthiliya zinazoingia sokoni, hufanya biashara kwa kuwalipisha wananchi
2. Pia kuonesha filamu zinaruhusiwa kuanzia saa 6 usiku
3. Vipindi vyenye haki miliki (mfano mpira wa ligi kuu Uingereza inayorushwa na DSTV pekee aliyeshinda zabuni)
Hivyo kilichokua kikifanyika, wengi walikua wanalipisha wananchi kwa maudhui yasiyostahili kulipiwa mfano DSTV mwaka 2017 waliiweka chanel ya Clouds ilihali akijua haruhusiwi kuiweka.
Mhandisi Mihayo alimaliza kwa kupokea ombi la kutoa semina hiyo kwa Baraza la Madiwani ambalo litakuwa tayari kuwaalika endapo watahitaji kuelewesha juu ya mada iliyotolewa.
Kwa upande wake Mhandisi wa Masafa Ofisi ya TCRA Kanda William Mnyippembe akawasihi walio na changamoto kuhusiana na kukosekana kwa TBC pekee kwenye visimbuzi vya Azam, DSTV na Zuku wawasiline na ofisi ya kanda ili wapate msaada.
Mhandisi Gabriel akihitimisha, amewapongeza TCRA kwa mapinduzi ya kiutendaji kwa kuhakikisha tunazalisha ajira kutumia mitambo iliyowekwa nchini lakini vilevile udhibiti wa kipindi na muda gani jambo lipi litoke liende kwa umma na kuwaasa wananchi kuwa waelewa na watulivu wakati mikakati ya mawasiliano inaimarishwa vilevile kwa lengo la kulinda usalama wa nchi. Pia amewakumbusha wananchi kuendelea kuangalia visimbuzi vya Star Times, Continental na Digitek ili kupata chaneli za ndani.
Mwisho kabisa, Mhandisi Gabriel akakabidhi leseni ya urushaji matangazo kwa chombo cha habari Storm Fm Redio kwa ajili ya Redio ya Mtandaoni (Online Radio) iliyopo Mjini Geita.
Semina hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Katibu Tawala Mkoa, Wahe. Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Makatibu Tawala Wilaya, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo bila kusahau Waandishi wa Habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa