Ni siku ya nane tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dtk. John Pombe Magufuli atangaze uamuzi wa kurejeshwa kwa utaratibu wa ulipaji wa mafao ya wafanyakazi wanaostaafu uliokuwa ukitumika kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi za jamii, na kutaka utaratibu huo utumike mpaka mwaka 2023 wakati wadau wakijadiliana juu ya kikokotoo kitakachotumika kulipa mafao hayo bila kuathiri mfuko na wastaafu kulipwa vizuri, hali inayopelekea Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi TUCTA Mkoa wa Geita kutembea kwa amani hadi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita kwaajili ya kufikisha pongezi kwa Mhe. Rais.
Akipokea Hati ya Shukrani na Pongezi hizo zilizoelekezwa kwa Mhe. Rais, baada ya kupokea matembezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.Mhandisi Robert Gabriel amewapongeza watumishi hao walioonesha sura za furaha kwa kutambua upendo alionao Mhe. Rais kwa watumishi akiwasisitiza kuongeza jitihada zaidi katika utendaji kazi ili kuendelea kuleta mabadiliko ndani ya mkoa, na taifa kwa ujumla.
Amesema, “nawapongeza sana TUCTA kutoa zawadi hii kwa Mhe. Rais, lakini kwa uvumilivu wenu mlipokuwa mkipitia wakati mgumu kabla ya maamuzi ya kiongozi wetu wa nchi. Mmeweka ahadi pamoja na shukrani hizo, kuwa mtafanya kazi kwa bidii, nawaomba muishi ahadi hiyo”.
Mhe.Mhandisi Gabriel amewaambia watumishi hao kuongeza hatua kazini, huku akisisitiza kuepuka rushwa kwani ni adui wa haki na kwamba watumishi ni vyema kuwajibika bila kujali umasikini au utajiri wa mtu ndipo taifa litaendelea, kisha akaahidi kufikisha ujumbe huo kwa Mhe. Rais na akajumuika kuimba wimbo pamoja na watumishi hao baada ya kupokea hati na tuzo (mfano wa ngao).
Akisoma maelezo yaliyopo kwenye hati hiyo kabla kuikabidhi, Mwl. John Kafimbi ambaye ni mratibu wa matembezi amesema, lengo la matembezi hayo ni kutoa shukrani kwa Mhe.Rais kwaniaba ya wafanyakazi wote Mkoa wa Geita kuruhusu kikokotoo cha zamani kuendele kutumika, huku wakiweka wazi kuwa, wamehamasika sana na juhudi za Mhe. Rais katika kuwathamini wafanyakazi wa nchi hii wakisema, ni matumaini yao kuwa majadiliano yatakayoendelea juu ya kikokotoo kipya yatajikita zaidi kuboresha maslahi ya wastaafu, kisha kuomba salamu hizo zifikishwe kwa Mhe.Rais.
Akikabidhi tuzo ya Mhe. Rais kwa Mkuu wa Mkoa, Martine Matiba ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa TUCTA Mkoani Geita amesema, kama watumishi wanaahidi kufanya kazi kwa bidii na hawatamuangusha Mhe. Rais katika utendaji kazi.
Miongoni mwa jumbe zilizoandikwa kwenye mabango yaliyobebwa na wayumishi ni pamoja na “Habari ya Kikokotoo Kwisha Kazi, Sasa Kazi Tu- CWT (M) Geita, Kikokotoo cha Sasa ni Full Amani Nyumbani, Kazini na Mtaani, Yeko Mkuu wa Kazi – TALGWU (M) Geita na Kikokotoo Sasa Raha, Wastaafu & Familia Zao-TAMICO (M) Geita”
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa