Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule ameeleza kusikitishwa kwake kwa namna ambavyo wengi wa maafisa Lishe ndani ya mkoa huo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao bila kufikia malengo jambo ambalo limechangia kuurudisha nyuma mkoa katika baadhi ya maeneo kwenye suala la lishe.
Hayo yameelezwa leo Februari 14, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Mwl.Julius Nyerere EPZA-Geita Mjini wakati Mhe.Senyamule akifunga kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Mkoa.
“kwakweli sijafurahishwa na mrejesho kutokana na tuliyoyaazimia kikao kilichopita, hivyo niombe mwende mkayafanyie kazi tuliyokubaliana kwakuwa kama mkoa tunataka kutengeneza kizazi cha watanzania wenye akili ya nyingi ya kutosha kutokana na lishe iliyo bora. Sasa mtambue tu ya kuwa, suala la lishe si ombi, si hiari bali ni wajibu wetu kutekeleza” alisema Mhe.Senyamule.
Vilevile Mhe.Senyamule amewaagiza wakurugenzi kuhakikisha wanatenga fedha ili kuwezesha shughuli za lishe kwenye halmashauri zao ili kufikia malengo, kisha kuipongeza halmashauri ya mji Geita kwa jinsi inavyojitahidi.
Baada ya kumaliza mjadala kuhusu lishe, Mhe.Senyamule amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Geita kuwawekea malengo maafisa chanjo wao ili waweze kuwasaidia wananchi kwa kuwahimiza kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19, lakini pia kuwahimiza walezi na wazazi kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwaajili ya kupata chanjo ili kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo Surua Rubela.
Awali, Bi.Riziki Mbilinyi ambaye ni Afisa Lishe Mkoa aliwasilisha tarifa ya utekelezaji ambayo ilionesha kuwa bado halmashauri nyingi za mkoa wa Geita hazijafanya vizuri hususan kipengele cha matumizi ya fedha kuwezesha shughuli za lishe.
Naye Afisa Chanjo wa Mkoa Bi.Wille Luhangija alitoa taarifa ya mwenendo wa utoaji wa Chanjo za kawaida kwa watoto na ile ya UVIKO-19 ambapo ilionesha kuwa, mwitikio umekuwa mdogo na kwamba jitihada zaidi zinahitajika kwa ushirikiano wa pamoja ili kuongeza idadi ya wachanjwaji. Vilevile alisisitiza kuwa mkoa unazo chanjo za kutosha aina nne za Sinopharm, Pfizer, Moderna na Johnson Johnson (JJ).Pia Luhangija ameongeza kuwa, mkoa umefanikiwa kuongeza vituo viwili vya chanjo ya UVIKO-19 katika hospitali ya Geita na Mgodi wa GGML.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakurugenzi, sekretarieti ya mkoa, waganga wakuu wilaya, waweka hazina, maafisa mipango na maafisa lishe wa mkoa wa Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa