Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalage ameeleza kufurahishwa kwake kwa jinsi ziara aliyoifanya ilivyozaa matunda kwa kutatua kwa pamoja changamoto iliyokuwa ikichelewesha kuanza kwa ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto (Maternity Block) tangu mwaka 2021 katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.
Hayo yameelezwa Februari 23, 2022 katika ukumbi mdogo wa mikutano kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita wakati wa kikao kazi kutafuta utatuzi wa changamoto zilizokwamisha Ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto.
Akiongea wakati wa kuhitimisha kikao kazi hicho, Dkt. Shekalage amempongeza Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Musa Chogero ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao kufuatia utendaji wenye kuleta matokeo, huku akihimiza uwazi, uzalendo, mawasiliano na mshikamano kwa wajumbe wakati wote mradi huo utakapoanza kutekelezwa ili kuwatendea haki wananchi wa Geita , Mhe.Rais na Wizara kwa ujumla kwani huduma hiyo ni muhimu sana.
“hongereni Geita kwa kumpata kiongozi huyu msikivu, ni mtu wa matokeo ndiyo maana wizara imemuamini. Lakini pia, niwaombe timu hii kuwa binafsi sitaki kuwa sehemu ya kufeli, kwahiyo tushikamane kwa pamoja ili mradi huu uanze kutelezwa mara moja na kuanzia tarehe 30 Machi, 2022 mkandarasi awe ameingia kazini”. Alisema Dkt. Shekalage.
Aliendelea kusema, “pamoja na hayo, bila mawasiliano yaliyojengeka vizuri hatutaweza kufanikisha utekelezwaji wa mradi huo. Hivyobasi tuwe wamoja, kwani mradi huu ni wetu sote, na mwisho tunatakiwa kutoa matokeo ya kitu kimoja, jengo la mama na mtoto”.
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw.Musa Chogero alimueleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa, mkoa umejiandaa kwenda na kasi kwenye utekelezaji wa mradi huo kwani ni hitaji kubwa la wananchi na ni vyema kuwa na matokeo ya haraka na kuwashauri wajumbe wa kikao hicho hususan wataalam kutoa mawazo ambayo yangeweza kutatua changamoto zozote ambazo zingeweza kujitokeza kutokana na aina ya utekelezwaji mradi iliyopendekezwa.
Kikao hicho kilowahusisha wataalam kutoka Wizara ya Afya na kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wakiwa kama wateja na wawezeshaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kupitia Katibu Tawala wa Mkoa kama msimamizi mkuu wa mradi wote, na Kampuni ya Crystal Consultants kama Mshauri Elekezi .
Kabla ya kikao kuanza, wajumbe wa kikao kazi hicho walizuru kwenye eneo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita na kuona majengo mbalimbali kisha kuona eneo litakapojengwa Jengo la Mama na Mtoto pamoja na kushuhudia uchimbaji wa msingi wa majengo ya Dharura (EMD) na la Wagonjwa Mahututi (ICU).
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima.
Boazi Mazigo
Afisa Habari
Geita RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa