Watendaji wa serikali mkoani geita wametakiwa kuhakikisha wanahamasisha usafi wa mazingira ili kuwaepusha wananchi na mbu waenezao Malaria ikiwa lengo la serikali ni kuwa na asilimia sifuri ya malaria ifikapo mwaka 2030.
Wito huo umetolewa na mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel oktoba 7, 2019 wakati akifungua kikao cha mapitio ya mradi wa uelimishaji na uhamasishaji wa jamii juu ya ugonjwa wa malaria mkoani geita lilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita.
Mhandisi Gabriel Amesema, “vita dhidi ya malaria tunaiweza, usafi wa mazingira hauitaji fedha za kigeni wala wataalamu kutoka nje ya nchi. Hivyo niwaombe tuhimize na kuhamasisha usafi pamoja na matumizi sahihi ya vyandarua vyenye viuwatilifu huku tukishirikiana na viongozi ili wanapopata nafasi ya kuongea kwenye mikutano, nao waweze kulisemea jambo hili”.
Mhandisi Gabriel ameishukuru timu ya Afya Mkoa kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Afya; TCDC, PSI, USAID Boresha Afya, Abt Associate, APHFTA na GGM katika mapambano na Ugonjwa wa Malaria kupitia afua mbalimbali katika Mkoa wa Geita na kufanya maambukizi ya malaria kupungua.
Imeelezwa kuwa, takwimu za malaria kutoka Tanzania Demographic Survey (TDHS) na Malaria Indicator Survey (MIS) zilionyesha kiwango cha mambukizi ya malaria nchini Tanzania Kushuka kutoka asilimia 14.1 kwa mwaka 2015/16 hadi asilimia 7.3 kwa mwaka 2017/18. Aidha kwa Mkoa wa Geita, utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) unaonesha kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kutoka aslimia 38.1 kwa mawaka 2015/16 hadi asilimia 17.3 kwa mwaka 2017/18 na kwamba Kupungua huko ni kutokana na juhudi kubwa ya Serikali katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama ilivyoelezwa hapo juu.
Kipekee, mhandisi Gabriel akamaliza kwa kuipongeza TCDC kuendelea kusaidia uelimisha wa Jamii juu ya Ugonjwa wa Malaria, athari zake na namna ya kupambana nayo; ikiwa ni moja ya njia kuu ya kuhakikisha wananchi wenyewe wanakuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Malaria. Pia amewashukuru TCDC kwa kuwezesha kufanikiwa kwa kikao hicho muhimu cha mapito ya mradi na kujadili mambo mbalimbali yatakoyowezesha kutoka hapa tulipo na kufikia kiasi cha chini ya asilimia 5% ambayo Mkoa umejiwekea na hatimaye kufikia aslimia 0% ambayo ni mpango wa Taifa ifikapo 2030.
Akitoa shukrani kwaniaba ya shirika lisilo la kiserikali la TCDC, Mkurugenzi Mkuu Deo Mwanansabi amesema, wao wanajisikia fahari sana kupokelewa na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita na anaamini kwamba, mradi huo ulioanza mwaka 2016 unaofikia ukomo mwaka huu 2019, uliyokuwa ukijumuisha halmashauri zote sita za mkoa wa geita, utaendelea kufanya kazi kutokana na elimu ilyotolewa kwa wataalam na jamii kwa ujumla na kwamba juhudi za wadau mbalimbali ndizo zitakazotokomeza ugonjwa wa Malaria.
“ZIRO MALARIA, INAANZA NA MIMI”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa