Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba (Mb) amekutana na kufanya kikao na viongozi mbalimbali wa serikali wa Mkoa wa Geita katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita alipokuwa katika ziara yake yenye ujumbe wenye fursa katika eneo la Hifadhi ya mazingira, kisha kutembelea kisiwa cha Magafu kilichopo Kijiji na Kata ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato tarehe 25.08.2018.
Waziri Makamba amepongeza kazi inayofanywa na Mkoa wa Geita chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ambayo imeendelea kuutangaza mkoa na kuuletea heshima. Pia amesema, amekuja mkoani Geita kwa madhumuni makubwa ya kupata maeneo ambayo yanaonekana kuwa ni nyeti na muhimu ya kiikolojia ambayo hayajatambulika ili yaweze kutambuliwa na kulindwa kwa maslahi ya kizazi kijacho kwa kushirikisha pia wananchi ili kupunguza malalamiko ya ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi.
Amesema, “kazi inayofanywa kwa sasa ni kuhakikisha tunalinda mazingira kwa ajili ya kizazi kijacho, kwani miongoni mwa sifa za kiongozi ni kutengeneza mazingira mazuri kwa vizazi vijavyo kwa miaka hamsini na kuendelea na si miaka miwili, mitatu”.
Amehimiza juu ya uwepo wa kamati za mazingira na watumishi wakaguzi wa mazingira na kuanzia ngazi ya sekretarieti ya mkoa hadi kitongoji ambao wataweza kufanya jukumu la hifadhi ya mazingira kutekelezwa kwa urahisi.
Ameongelea pia juu ya mpango wa kusogeza huduma za hifadhi ya mazingira kupitia kifungu 26 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, Na. 20 ya Mwaka 2004 kinachosema kuwa “kwa kuzingatia Sheria hii, Baraza linaweza kukasimu kwa Wizara ya kisekta, chombo cha usimamizi wa mazingira, mwajiriwa au wakala wa Baraza, madaraka yoyote au majukumu ya Baraza chini ya Sheria hii” na kwamba hii itaweza kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Kisha Mhe. Waziri alielekea Wilayani Chato katika Kata na Kijiji cha Nyamirembe akasomewa taarifa kisha kuongea na wananchi wa eneo hilo na kusikiliza kero walizonazo juu ya hifadhi ya mazingira na baadaye kutembelea kisiwa cha Magafu kilichopendekezwa na wanachato ili kingie katika utaratibu wa kutangazwa kuwa eneo la hifadhi kwani ni eneo muhimu kwa utalii na mazalia ya samaki hivyo kuona ni muhimu kuendelea kutunza eneo hilo kwa ajili ya vizazi vya baadae.
Jambo la pekee akiwa anaongea na wananchi ni pale alipojitokeza binti mmoja aliyeomba kupata msaada wa kupewa viongozi watakaowaelekeza vyema wasiojua kusoma na kuandika yeye akiwemo akiwa anatoa machozi, jambo lilipelekea Mhe. Waziri kumsaidia binti hiyo ili aweze kwenda shuleni.
Waziri Makamba baada ya kufika Magafu aliridhika na mvuto na uzuri wa eneo hilo kisha kuahidi kuleta wataalamu wa mazingira ndani ya wiki tatu kuja kujihakikishia kitaalamu mambo yanayotakiwa kuzingatiwa ili mchakato wa kurasimisha zoezi hilo ukamilike mapema kisha kuahidi kutafuta wadau wa kuwezesha suala zima la ulinzi kufanikiwa kwa kuwa linahitaji rasilimali mbalimbali ikiwemo mafuta kwa ajili ya boti za doria.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mhe. Christian Manunga naye akasisitiza juu ya uchumi utakaotengenezwa kupitia hifadhi ya kisiwa asilia cha Magafu hicho kutokana na kuwa ni mazalia ya samaki hivyo akaomba ulinzi uanze mara moja ili asitokee mtu kwenda kufanya shughuli yoyote.
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Mhandisi Mtemi Msafiri akachukua fursa hiyo kumweleza Mhe. Waziri kuwa kisiwa hicho ni muhimu Kwa ustawi wa jamii ya wanachato, na kwa kuwa kisiwa kipo karibu na hifadhi ya Taifa ya Rubondo, basi ikipendeza hata hoteli ya kitalii kujengwa humo kwa baadae itakua ni moja ya kukuza uchumi, hivyo ataendelea kuimarisha ulinzi na kuanza jitihada za kukiifadhi mapema iwezekanavyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel alimpokea mhe. waziri na baada ya kikao kuisha, Mkuu wa Mkoa alishukuru kwa ugeni huo na kuahidi kutekeleza yote yaliyoagizwa ikiwemo kupata orodha ya maeneo pendekezwa kwa kuhifadhiwa lakini pia watumishi pendekezwa ili wateuliwe kuwa maafisa wakaguzi wa mazingira. Kipekee Mkuu wa Mkoa alitoa dhamira ya mkoa kushika nafasi ya ndani ya tatu bora kwa utunzaji mazingira hivyo uwepo wa Mhe. Makamba ni kuamsha hamasa kwa mkoa.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa, ndugu Herman Matemu alisoma taarifa ya mkoa iliyofuatiwa na dhumuni la ziara kutoka kwa mhe. Waziri.
Naye Mbunge wa Nyang’hwale Mhe. Hussein Amar Nassor akashukuru kwa niaba ya viongozi walioshiriki kikao cha Mhe. Waziri na kumpongeza Mhe. Makamba kwa kujitolea kuiletea Geita fursa hizo adhimu.
Kikao cha Mhe. Waziri kilihudhuriwa na Wahe. Wakuu wa Wilaya, Wahe. Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Maafisa Mazingira wa Halmashauri, Afisa Madini Mkazi, Wawakilishi wa NEMC kanda ya Ziwa n.k
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa