Mafunzo ya Ufuatiliaji (Traceability) uzalishaji wa Dhahabu yatawainua wachimbaji wadogo kwa kuwaweka pamoja wadau wote walio katika mnyororo wa thamani kunufaika na bidhaa inayozalishwa.
Hayo yamebainishwa tarehe 02/08/2024 wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa Maafisa wa Serikali kutoka Idara wezeshi za uchimbaji dhahabu Mkoa wa Geita na Halmashauri husika, Viongozi wa vyama vya wachimbaji wadogo ngazi ya mkoa na wilaya ambazo mradi unatekelezwa ambayo yamelenga kujenga uelewa kwa watu hao kama nyenzo muhimu.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndg. Mohamed Gombati ametoa shukrani za dhati kwa shirika la SOLIDARIDAD kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu ambayo yatawaongezea Maafisa wa Serikali na wachimbaji wadogo uelewa wa nyenzo inayotumiwa na Shirika hilo kufanya ufuatiliaji na tathmini ya migodi.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kuifanya sekta ya madini kwa wachimbaji wadogo kuwa wenye tija, inayojali jamii na rafiki wa mazingira, ambapo Mradi unalenga kuwafikia wanufaika 9,000 wa moja kwa moja na 18,000 wasio wa moja kwa moja..
“Mbinu na mikakati inayotumiwa na mradi ili kufikia lengo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wachimbaji, mafunzo kwa viongozi wa wachimbaji kwa kutumia wataalam husika na vyombo vya habari pamoja na kuwaunganisha wachimbaji wadogo na wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa dhahabu.” Aliongeza Ndg. Mohamed Gombati.
Meneja Mradi wa Shirika la SOLIDARIDAD lenye makao makuu yake Mkoani Arusha Bi. Winfrida Kanwa ameeleza kuwa shirika lake linatekeleza miradi miwili ambayo ni Pathways To Prosperity ambao ni mradi wa miaka 7 ulioanza mwaka 2023 na utamalizika mwaka 2029, Mradi huu unatekelezwa katika mikoa miwili ya Geita na Shinyanga ambapo jumla ya migodi 60 ikiwemo 45 ya Mkoa wa Geita ni wanufaika.
Bi. Winfrida Kanwa amesema kuwa mradi mwingine ni Realizing the Potential of Responsible ASGM trade. Mradi huu ulioanza mwaka 2021 unatekelezwa katika Mkoa wa Geita na umeweza kuifikia migodi 10 ukiwa na lengo la kuwaunganisha wachimbaji wadogo na wadau mbalimbali ili waweze kupata taarifa za kijiolojia, masoko mazuri na wafanye matumizi salama ya zebaki pia wapate njia mbadala wa zebaki.
Halmashauri za Wilaya katika Mkoa wa Geita ambazo zinanufaika na mradi ni pamoja na Bukombe, Chato, Geita na Nyang’hwale.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa