Katika kipindi cha miezi michache ijayo kabla ya kumalizika kwa mwaka 2024 Shirikisho la Machinga Mkoa wa Geita (SHIUMA) litanufaika na Ofisi ya kisasa iliyopo katika mtaa wa Bombambili Kata ya Bombambili Halmashauri ya Mji Geita ambapo kwa sasa ujenzi ujenzi wa Ofisi hiyo umefikia zaidi ya asilimia 85% kwa kazi za ndani na nje.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Ofisi hiyo mbele ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Ndg. Felister Mdemu alipotembelea kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hiyo tarehe 21/08/2024, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Mji Geita Bi. Mariam John ameeleza kuwa upatikanaji wa ofisi hiyo utakuwa na manufaa kwa viongozi wa machinga pamoja na wajumbe wao kupata sehemu rasmi na rafiki kwa ajili ya kufanyia kazi tofauti na hali iliyokuwepo awali.
Bi. Mariam John amesema kuwa Ofisi inayojengwa itachukua watoa huduma wawili na wageni wanne badala ya mtoa huduma mmoja na wageni wawili kama mchoro wa awali ulivyokuwa ukianisha. Pia Ofisi ina ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 20 badala ya kumi waliokuwa wameainishwa hapo awali.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa machinga katika jamii anayoiongoza na kutoa Shilingi milioni 10 kwa kila mkoa kwa ajili ya kuanzisha ujenzi huo ili wajasiriamali hao wapate mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Ndg. Felister Mdemu ameipongeza Halmashauri ya Mji Geita kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo pamoja na kuongeza fedha nyingine kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri ili ofisi hiyo iweze kukamilika na kuanza kutoa huduma, sambamba na usimamizi mzuri unaofanywa na wahandisi wa Halmashauri katika kuhakikisha jengo hilo linajengwa kwa viwango vinavyokubalika.
Ujenzi wa Ofisi ya Shirikisho la Machinga Mkoa wa Geita ulianza rasmi tarehe 09/06/2023 ambapo katika awamu ya kwanza kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa msingi, ujenzi wa boma, ujenzi wa nguzo wima na mlalo, uchimbaji wa shimo la maji taka pamoja na kazi nyingine za awali za ujenzi. Mpaka kufikia tarehe ya ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii jumla ya Shilingi 27,053,180 zimekwishatumika.
Ujenzi wa Ofisi ya Shirikisho la Machinga Mkoa wa Geita umetokana na ahadi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa viongozi wa shirikisho hilo jijini Dodoma mnamo tarehe 16/05/2022 walipokuwa kwenye mafunzo ya uongozi na fursa kiuchumi ambapo Mhe. Rais aliahidi kutoa Shilingi Milioni 10 kwa kila mkoa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi hizo na akatekeleza.
Kwa mujibu makadirio ya kihandisi, ujenzi wa Ofisi ya Shirikisho la Machinga Mkoa wa Geita utagharimu jumla ya shilingi 54,443,108.67/= ambapo utajumuisha ujenzi wa jengo la ofisi lenye vyumba vitatu pamoja n ukumbi, Ujenzi wa choo cha matundu matatu ikijumuisha mifumo ya maji, mashimo ya maji taka pamoja na tenki la kuhifadhia maji na kitako chake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa