Ni kauli ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Bw. Denis Bandisa, alipokutana na kufanya mazungumzo na Watumishi wa Halmashauri ya Wilya ya Bukombe katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 07.09.2018 alipokuwa kwenye ziara ya kikazi akijitambulisha kwa watumishi na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa.
Bw. Bandisa ameanza kwa kuipongeza Bukombe kwa namna ambavyo imekua Halmashauri ya mfano kwa utunzaji wa mazingira kupitia utaratibu waliojiwekea wa marufuku ya ukataji wa miti hovyo. Amewaeleza watumishi hao kuwa pamoja na yeye kujitambulisha kwao, pia anaendelea kukumbusha watumishi juu ya uadilifu kwenye utumishi wa umma.
Amesema, “nawapongeza kwa nidhamu mlioionesha hata kwa kuitikia wito wangu, lakini pia niwakumbushe kuwa mnatakiwa kuzingatia mkataba wenu na mwajiri mkijua ya kwamba, kwakuwa mlikubali kuja kufanya kazi Bukombe basi mkubali kuwajibika na mtambue kuwa Rushwa kwa mtumishi wa Umma ni Hapana kwa kuwa inatoa upendeleo wa utoaji huduma na mkiipenda rushwa, hamtamaliza utumishi wa umma, mtakamatwa tu siku yoyote”. Amempongeza pia Mkurugenzi wa Halmashauri, Bw. Dionis Myinga kwa namna anavyowasimamia watumishi hao.
Bw. Bandisa amewakumbusha wanabukombe kuhakikisha wanatatua migogoro midogomidogo ya ardhi ambayo mingi hupelekea migogoro mikubwa, hivyo awashauri kulipa fidia mara moja wanapoyatwaa maeneo ili kuruhusu maendeleo kufanyika.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato amesema kwamba, bado halmashauri inaweza kukusanya zaidi, hivyo wahakikishe mifumo inafungwa kuanzia kwenye zahanati, kituo cha afya mpaka hospitali na iingiliane na mifumo ya benki ili kujua makusanyo yaliyopatikana, hiyo itapunguza mianya ya upotevu wa mapato. Lakini aonya wanaocheza na mashine za kukusanyia mapato kielektroniki (POS) na kuwataka wahakikishe wanakusanya kwa uaminifu.
Ameeleza pia juu ya halmashauri kuhakikisha inatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kabla ya kufanya matumizi kwa kuzingatia asilimia 4 vijana, asilimia 4 wanawake na asilimia 2 wenye ulemavu kwa kuwa haya ni makato ya kisheria (statutory deductions) hivyo ni lazima kuzingatia lakini kuhakikisha wanasimamia fedha hizo zinapokopeshwa ziweze kurudi ili na wengine wanufaike nazo.
Mwisho akawakumbusha watumishi hao juu ya kujali afya zao kwa kuzingatia mlo na kufanya mazoezi bila kusahau kujiepusha na mambo yanayoweza kuhatarisha afya kwa ujumla na kumalizia kwa kusema, “utendaji kazi wenu uwe wa kutukuka unaozingatia Sheria, Taratibu na Kanuni (STK)”.
Afisa vijana kwa niaba ya Afisa Elimu wa Mkoa Bi. Lilian Lwegoshola akawakumbusha watumishi hao kuhakikisha kunakuwepo na taarifa zisizokinzana lakini pia fedha asilimia 10 za mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu zinatolewa na kurudishwa kwa wakati.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa Bw. Peter Tango akawakumbusha watumishi hao kuwahimiza wananchi kuendelea kushiriki ujenzi wa miundombinu ya afya kwa kutambua kuwa bado wanao uhitaji wa huduma hiyo muhimu.
Katibu Tawala Msaidizi, Serikali za Mitaa Bi. Sania Mwangakala akatumia fursa hiyo kuwakumbusha juu ya kuzingatia ushauri wa Sekretarieti ya Mkoa juu ya masuala mbalimbali yanayojitokeza, kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano na mshikamano kwa kuwa kazi zote hufanywa kwa kutegemeana na pia kufanya kazi kama wamoja na endapo atakwama mtu ni vyema aombe msaada. Mwisho awasisitiza juu ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za kieletroniki.
Akifunga kikao hicho na kushukuru kwa niaba ya watumishi wa umma Bukombe, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Paul Cheyo amesema, watumishi wa Bukombe, wanaahidi kutekeleza maelekezo yote waliyopewa na kisha baadhi ya watumishi na Katibu Tawala Mkoa wakaambatana kutembelea baadhi ya Miradi ya Elimu na Afya ikiwemo uboreshaji wa Kituo cha Afya Ushirombo (Ujenzi wa Maabara, Wodi ya Mama na Mtoto, Nyumba ya Mtumishi na Nyumba ya Kuhifadhia Maiti (Mortuary) na Shule ya Sekondari ya Businda (Ujenzi wa Vyumba 3 vya madarasa, matundu 8 choo cha wavulana na matundu 8 choo cha wasichana).
Katibu Tawala Mkoa wa Geita ataendelea na ziara yake katika Halmashauri za Chato na Mbogwe.
Geita: Amani, Umoja na Kazi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa