Takribani vijana 4,000 nchini Tanzania wanatarajiwa kufikiwa na Mradi wa Mafunzo ya Ujasiriamali kwa Vijana Juu ya Uendeshaji, Ubunifu wa Biashara yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia taasisi yake ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Timu ya Watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira, Wenye Ulemavu na Wadau Wengine,
Hayo yameelezwa na Mhe.Jenista Mhagama (Mb) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, wakati akifungua mafunzo hayo kwa vijana washiriki takribani 150 ndani ya Mkoa wa Geita Agosti 24, 2019 katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita akiongea na vijana wa Geita Kwaniaba ya Vijana wa Tanzania huku akisisitiza juu ya umuhimu wa serikali ya mkoa kuhakikisha vijana watakaopokea mafunzo hayo wanaleta matokeo chanya lakini vilevile vijana wenyewe kuhakikisha wanakuwa chachu kwa wenzao.
“vijana mnaopata mafunzo haya tumshukuru Mhe.Rais Magufuli kwani kupitia serikali anayoiongoza amenituma kufungua mafunzo haya ili kuwandoa kwenye fikra potofu za kukaa kijiweni kutegemea mambo makubwa bila kufanya kazi, vilivile kuwaeleza vijana msiendelee kutokufanya maamuzi mnapokutana na maelekezo ambayo yanaweza kuwapatia fursa katika maisha yenu, hivyo nafarijika kupata fursa kama waziri mwenye dhamana kufungua mafunzo haya. Hivyo ni vyema serikali ya mkoa ihakikishe vijana wanafuatiliwa kwakuwa fedha zilizotumika ni kutokana na kodi za wananchi na tunataka yawe ni kati ya mafunzo yenye matokeo chanya yatakayoleta mabadiliko nchini kupitia vijana wa wilaya za mkoa wa geita”, alisema Waziri Mhagama.
Vilevile Waziri Mhagama amewataka vijana hao kuongeza idadi wakiwafundhisha vijana wengine elimu watakayoipata ili vijana wote watanzania waweze kufikiwa na kubadilika, kwani wao wanao uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa wakijenga uchumi huku akiwasihi kuyaishi maisha ya Hayati Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere aliyeutumia ujana wake kuupigania uhuru wa taifa kwa kujitolea kuacha kazi na kuingia kwenye mapambano ya kutafuta uhuru wa nchi hii pamoja na maendeleo kwa ujumla, kisha kuwapongeza wabunge wote kwani wao ndiyo walioidhinisha fedha zilizowezesha mradi huo bila kumsahau Mkuu wa Mkoa Eng.Robert Gabriel kwa kutambua shughuli zinazofanywa na ofisi yake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amewakumbusha vijana kutumia mafunzo hayo kuja na mipango madhubuti ya kujiajiri itakayowafungulia milango ya kiuchumi wakati wa utekelezaji mradi wa bomba la mafuta linalotoka Ohima Uganda hadi Tanga kwani miongoni mwa maelekezo ya serikali ni kwamba, wananchi wanatakiwa kuumiliki na kuushiriki uchumi wakiujenga kwa kuuza bidhaa na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo vyakula ambayo hiyo ni fursa kubwa, hivyo wanapaswa kuitumia bila kusahau kuyatumia vizuri makundi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp kuhabarishana kuhusu maendeleo na fursa mbalimbali ili kujinufaisha kiuchumi, na kumaliza kwa kukabidhi vyeti kwa washiriki 52 ambao wamekwishapata mafunzo hayo.
Mhe. Hamim Gwiyama, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale ambaye ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa amewaeleza vijana hao kuwa, uwezo wa kuboresha maisha upo mikononi mwao kwakuwa fursa ni nyingi, hivyo ni imani yake kuwa elimu hiyo itawaamsha akisema “tuzingatie maagizo ya Mungu ya elimu, ibada na kazi, kwamba, asiyefanya kazi na asile na asiye na maisha mazuri anapaswa kujilaumu mwenyewe na muepuke vijiwe vya drafti” kisha kuwashauri kuzalisha hata kwa kufuga wakianzia kuku mmoja anayeweza kutotoa vifaranga 12.
Kwa upande wake Bi. Beng’i Issa ambaye ni Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) amesema, hadi Agosti 24, 2019, jumla ya vijana 426 wameshanufaika na mafunzo haya katika mikoa ya Dodoma, Ruvuma na vijana 52 kutoka Mkoani Geita. Pia, vijana wengine 103 kutoka mkoani Geita watanufaika na mafunzo haya kuanzia leo Agosti 24, 2019 ambapo vijana 50 watashiriki katika mafunzo haya kwa siku 3 kuanzia leo tarehe 24 hadi tarehe 26, Agosti, 2019 na baadaye vijana waliobaki 53 watashiriki mafunzo haya kuanzia tarehe 27 hadi 29 Agosti, 2019, idadi iliyotokana na mwitikio mkubwa wa vijana kutokana na ushirikiano kutoka mkoa wa geita.
Pia Bi. Beng’i amesema, mafunzo hayo yatatekelezwa kwenye mikoa 8 ya GeIta ikiwa ni mkoa wa tatu, Lindi, Ruvuma, Mbeya, Arusha, Tanga, Dodoma na Mwanza. Mafunzo haya yatawanufaisha vijana 1,200 katika mikoa hii nane na yanatarajiwa kunufaisha jumla ya vijana 4,000 hapa nchini baada ya kuwafika vijana wa mikoa 18 iliyobaki ambayo haitashiriki kwenye awamu hii ya mafunzo na kuwaomba vijana kutoa taarifa zao sahihi ili kuwezesha ufuatiliaji
“ninaomba nikuhakikishie kuwa, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi litaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulumavu katika kuratibu utekelezaji wa programu za ukuzaji wa ujuzi kupitia mafunzo ya ujasiriamali”, alimaliza Bi. Beng’i kisha kuwashukuru wadau ambao wameshiriki pamoja hadi sasa katika kutekeleza mafunzo hayo ikiwemo mifuko ya Uwezeshaji ya Serikali (PASS Trust, SELF MF, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mfuko wa Misitu- TaFF), SIDO, TMDA, TBS, OSHA, TRA pamoja na taasisi za fedha kama vile Benki ya NBC, CRDB na NMB
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa