Na Boazi Mazigo, Geita-RS
Katika kuhakikisha mkoa unafikia malengo katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe, viongozi wa dini wameendelea kuhamasishwa kuwasaidia waumini wanaowaongoza ili watekeleze afua hizo kwakuwa kwao ni rahisi kufikisha ujumbe.
Wito huo umetolewa Oktoba 25, 2023 wakati wa kikao cha kamati jumuishi ya lishe kujadili utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha julai-septemba, 2023 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa Geita.
Akiongea wakati akifungua kikao, wa majadiliano na akifunga kikao, kaimu katibu tawala mkoa Geita Dkt.Omari Sukari alisema, ni muhimu kwa wajumbe kutoka kila sekta kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kupitia maeneo yao ili kufikia malengo katika utekelezaji wa afua za lishe huku akimpongeza Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentekoste TMRAC Mjini Geita Stephano Saguda kwa kuokoa maisha ya mwanafunzi mmoja aliyeletwa kanisani kwake kwa ajili ya maombezi ilihali ana shida ya lishe pasipo mzazi wake kujua.
“niwasihi wajumbe wote, kila mmoja kwenye eneo lake asaidie ufanikishaji wa afua za lishe kwa kutoa elimu, halmashauri nazo ziendelee kutoa fedha, lakini pia viongozi wa dini kama alivyotoa ushuhuda Askofu Saguda, tuwasaidie waumini ili wapate njia sahihi ya tiba wanapopatwa na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la lishe” alisema Dkt.Sukari.
Dkt. Sukari alimaliza kwa kutoa wito kwa jamii kujitahidi kuzingatia lishe kwa kuwa na bustani za mbogamboga na matunda angalao kila kaya ili kusaidia watoto kuwa na lishe nzuri.
Naye Askofu Stephano Saguda wa Kanisa la Pentekoste TMRAC Mjini Geita alisema, kama kiongozi wa Imani anaona kuna umuhimu mkubwa wa viongozi wa dini kuwasaidia wananchi kwani bado kuna imani potofu na wengi hukimbilia kanisani lakini kumbe pengine ana ugonjwa unaotibika akitoa ushuhuda kuwa, aliwahi kuletewa mwanafunzi mwenye hali mbaya ili aombewe apone, lakini alimshauri mzazi wa mtoto yule kuwa baada ya kumuombea atampeleka hospitali na ndipo iligundulika kuwa mtoto yule hakuwa na kingine isipokuwa shida ya lishe, kisha akatibiwa na anaendelea na masomo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha Januari hadi Septemba, 2023, Bi.Naomi Rumenyela ambaye ni afisa lishe mkoa alisema, miongoni mwa changamoto za utekelezaji ni mkoa kuwa na idadi kubwa ya watoto wa umri chini ya miaka mitano waliodumaa Zaidi ya kiwango cha taifa 38.6% licha ya uwepo wa ardhi na hali ya hewa inayoruhusu uzalishaji wa vyakula na kwamba wanaendelea kutoa elimu ya lishe katika jamii ili kuongeza uelewa wa masuala ya lishe.
Mwisho, wajumbe wote walikubaliana kutekeleza maazimio ya kikao hicho na kuleta mrejesho chanya kwenye kikao kijacho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa