Na Boazi Mazigo, Geita
April 03, 2019
Wachimbaji wa madini ya dhahabu kutoka nchini Uganda wameaswa juu ya kuwa na ushirikiano ulio mzuri baina yao na serikali kwani ndiyo mlinzi pekee wa mali za zao na za nchi kwa ujumla na kwamba kwa kulipa kodi na kutotorosha madini kutaimarisha uchimi wa nchi yao kama ambavyo Tanzania imeonesha mfano.
Hayo yameelezwa jana Aprili 3, 2019 na Waziri wa Madini wa Uganda Peter Lokeris kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wa Uganda alioambatana nao kwenye msafara wake, alipokuwa akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa serikali ya mkoa wa Geita wakati wa kuhitimisha ziara yao ya siku 4 nchini Tanzania, ambapo ameeleza kufurahishwa na ukarimu wa watanzania huku akiupongeza na kuushukuru uongozi wa serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini kwa namna walivyowaweka pamoja wachimbaji wake.
“kwanza niwashukuru watu wa jamhuri ya Tanzania, Rais wenu na serikali yote ya Tanzania kwa kuonesha mfano bora kwa kila hatua kwa kila mtu. Watu wa hapa ni wakarimu, hata nchi yetu ipo hivi ilivyo kutokana na msaada wenu kwakuwa viongozi wetu wengi walipewa msaada wa mawazo na ubunifu kutoka kwa Hayati Mwl. Nyerere, hongera” alisema Waziri Lokeris.
Akiendelea kusema, Lokeris alieza kuwa, awali kabla ya kuwashirikisha wachimbaji hao katika kutekeleza takwa la katiba ya nchi yao kwamba, madini humilikiwa na serikali hivyo ni namna gani wawaunganishe wachimbaji na serikali, ili serikali ipate mapato yake, na wachimbaji wapate sehemu yao ulikuwepo uadui kati ya serikali na wachimbaji, lakini baada ya kuwashirikisha sasa wamekuwa marafiki, sasa wanaweza kusema na kushaiuri bila woga.
Lokeris alimaliza akiwaambia wachimbaji hao kuwa “sasa tumejifunza kwa Watanzania, ni muhimu kutoikimbia serikali kwani ndiyo inayokulinda, ukikimbia na madini uliyonayo halafu yakaibiwa huwezi kwenda kuripoti polisi, utaogopa. Hivyo tujue unapoishirikisha serikali wakati umepata dhahabu yako, hakika italindwa, wewe utalindwa, serikali itapata mapato kwa kuimarisha uchumi na itakujengea miundombinu mbalimbali”.
Naye Mshauri Mwandamizi wa Rais wa Uganda, Getrude Njuba akatumia fursa hiyo kuwaeleza wachimbaji walioambatana nao kuwa, siku zote wananchi/watu huanzisha jambo kabla ya serikali akimaanisha kwamba, kama serikali haitajua mahitaji yao ni vigumu kuyakidhi akitoa mfano kuwa, awali wachimbaki hao waliitwa wavamizi migodini, lakini sasa wananitwa wachimbaji wadogo wadogo. Hakuishia hapo, Njuba aliendelea kusema kuwa, hata unapolinganisha msaada wanaoutoa kwa wachimbaji wa Uganda na ule wa Tanzania kwa wachimbaji wadogo, Serikali ya Uganda nayo inawathamini wachimbaji wadogo na ndiyo maana imefanikisha ziara hii nchini Tanzania kisha kushukuru uwakilishi mzuri wa uongozi unaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia ushiriki mzuri wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Alhaj Said Kalidushi.
Mbunge wa Kassanda Kaskazini kutoka wilaya ya Kassanda nchini Uganda, Nsamba Patrick Oshabe naye hakusita kueleza furaha yake juu ya ziara iliyokidhi shauku yake kama kiongozi wa eneo yanapochimbwa madini ya dhahabu kwa wingi huku akisema, “hiki ndicho nilichokuwa nikikipigania, nawashukuru wizara ya madini Uganda na Tanzania. Nimefurahi kumuona mwenyekiti wa CCM wa Mkoa ikimaanisha yupo anaangalia utekelezaji wa ilani kuanzia siku tumefika hapa Geita,hongereni sana”
Oshabe amesema, wamejifunza mambo mengi mazuri ikiwemo uhusika wa wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya serikali wakati wa uzalishaji dhahabu ikiwemo Jeshi la Polisi, TRA, Halmashauri, Ofisi za Madini na ya Usalama kwani kwa kufanya hivyo serikali hupata mapato stahiki hivyo wataiga mfano huo.
Mhandisi wa Sehemu ya Uongezaji Thamani wa Madini Assa Mwakilembe kwaniaba ya Wizara ya Madini na Mkuu wa Wilaya ya Geita Josephat Maganga kwaniaba ya Serikali ya Mkoa wakawatakia safari njema wageni hao wakiwaeleza kuwa, watanzania pia watakwenda kujifunza juu ya mafuta nchini Uganda hivi karibuni ikiwa ndipo mradi mkubwa unatokea, hivyo wasisite kuwapokea watakopkwenda kujifunza nchini mwao.
Katika ziara yao, walitembelea maeneo mbalimbali kujifunza ikiwemo Soko la Dhahabu Geita, Mgodi wa Mfano wa Serikali-Rwamgasa, Mgodi wa Busolwa-Nyarugusu Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM), kiwanda cha uchenjuaji dhahabu kiitwacho Rich Hill Elution Plant kilichopo eneo la Mpomvu Mjini Geita na kujionea hatua zote za uzalishaji wa madini ya dhahabu n.k
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa