Katika kuitimiza ndoto ya Mkoa wa Geita kuwa mkoa wa uwekezaji kimkakati, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameendesha kikao na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani ya mkoa wakiwemo viongozi wa Chemba ya Wafanyabishara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) tarehe 15.11.2018 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita.
Akifungua kikao hicho, Mhandisi Gabriel ameanza kwa kuwashukuru wadau hao kwa kuacha shughuli zao na kuja kutafakari kwa pamoja namna ya kuzitumia fursa zilizopo huku akiwaambia wadau hao kuwa wao ndio watakaoiinua Geita kwakuwa kila ndoto ina muotaji.
Amesema, “mageuzi yoyote yana waasisi, hivyo ninyi ni waasisi wa Geita mpya kwa kuwa Geita tunayooihitaji inahitaji mawazo yenu. Nakifananisha kikao hiki kama vile kiu ya mchungaji kuona watu wanaokoka baada ya kuhubiri mda mrefu, nikifananisha na jinsi mtakavyoleta maendeleo”.
Mhandisi Gabriel ameendelea kueleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuwa na Geita iliyoendelea na watu wake wakiwa wameendelea akiwaeleza wajumbe juu ya kuanzisha kumbi kubwa za mikutano, hoteli za kimataifa kwani Geita itakua na ukanda wa uwekezaji vilevile kuwa na maonesho endelevu ya kitaifa hivyo itakuwa na ugeni mkubwa na ni vyema fursa hiyo kuitumia.
Akihitimisha kikao hicho, mhandisi Gabriel ameeleza matarajio yake kwamba anategemea uwepo wa viwanda vya samaki, nyama, asali, uimarishaji wa soko la dhahabbu ikiwemo kuanzisha soko la dhahabu, bila kusahau uwekezaji kwenye maeneo ya kupumzikia.
Katibu wa CCM Mkoa Ndg. Adam Ngallawa kwa upande wake ameshukuru jitihada za Mkuu wa Mkoa na kuwaeleza bayana wajumbe wa kikao kuwa “sisi ndiyo tutakaoibadilisha Geita, hivyo tutumie fursa hiyo kujipanga kuondokana na mawazo madogo na twende kimataifa”.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Josephat Maganga akatoa uzoefu alioupata kwenye ziara Jijini Dar es Salamaa walipozulu kituo cha uwekezaji huku akisema Geita tunatakiwa kuzitumia fursa tulizonazo.
Miongoni mwa wadau wakubwa walioshiriki ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kusahau taasisi za kifedha za mkoa huu za CRDB, NMB na NBC ambao wote walionesha utayari wa kuwakopesha wafanyabiashara, lakini TADB wakasisitiza zaidi juu ya uwasilishaji maandiko ya kilimo ili miradi hiyo iweze kufadhiliwa.
Baada ya majadiliano, wadau walihamasika na waliweza kusema ndoto zao huku mmoja akisema yeye baada ya kikao hicho atapenda kupata eneo kubwa ili ajenge uwanja wa michezo huku wengine wakijielekeza kwenye usafiri wa mabasi ya kisasa na wakiomba kuharakishwa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami inayounganisha Geita na Kahama-Shinyanga kwakuwa kwa sasa changamoto ni barabara.
Katika kikao hicho imeelekezwa pia kuwa kila Wilaya ihakikishe inachangia uimarishwaji wa TCCIA ikiwa wao ndio kiungo kikubwa baina ya serikali na wafanyabiashara/sekta binafsi yenye mchango mkubwa kimaendeleo.
Mwenyekiti wa TTCIA Geita Eng. Chacha Wambura akawaeleza wajumbe kuwa mkoa umepata kiongozi na ni vyema wamtumie kwakuwa ana ndoto ya kuuvusha mkoa na wasimuangushe.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Wahe. Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Geita, wakurugenzi, maafisa biashara, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali za Umma yakiwemo Tanesco, bila kusahau Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na sekreatariet ya mkoa iliyowakilishwa na idara ya uchumi na uzalishaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa