Ikiwa zimebaki siku 11 kuelekea Maonesho ya kwanza ya Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji wa Madini ya Dhahabu yatakayofanyika Mjini Geita katika Uwanja wa CCM Kalangalala, wadau na wamiliki wa makampuni yanayojishughulisha na uchimbaji na uzalishaji wa madini ya dhahabu wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 12.09.2018 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa lengo la kufanikisha maonesho hayo .
Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amewashukuru wadau hao kwa namna ambavyo wamekuwa chachu kubwa ya maendeleo ndani ya mkoa na kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais kwa kufanikisha matukio mbalimbali ndani ya Mkoa yakiwemo uokozi kwenye migodi, uchangiaji madawati, ufanikishaji Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ujenzi wa nyumba za watumishi, ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya n.k. Amewaeleza wadau hao kuwa wanapaswa kutambua kuwa, maonesho hayo ni kwa ajili yao na wana Geita kwa ujumla na si yake hivyo ni muhimu kwa wao kushiriki kwa sababu watapata suluhu ya masuala mbalimbali ambayo wamekuwa wakikumbana nayo kama changamoto katika shughuli zao za uzalishaji, lakini pia watakutanishwa na makampuni yenye teknolijia bora ya uzalishaji hivyo wasipange kukosa.
Amesema, “maonesho haya ni ya kihistoria, hivyo tambueni ya kwamba, msimu wa dhahabu hautegemei mvua wala kiangazi, hapana uko palepale, hivyo tunapouangalia uchumi kwa Geita hatupaswi kujilinganisha na wengine wanaotegemea mvua, yatupasa tutambue umuhimu wa ushiriki wetu katika kuyafanikisha maonesho haya yatakayohudhuliwa na viongozi mbalilmbali wa serikali, makapuni ya kimataifa n.k”. Kubwa zaidi ameeleza nia ya serikali inayolenga utajiri wa rasilimali madini ulipo nchini uweze kuleta mapinduzi chanya kwenye maisha ya watanzania. Ameongeza akisema, “ningependa shughuli zenu zionekane, wenye mchanga wa madini leteni, wenye dhahabu njoo nazo, Masonara njooni mfanye biashara ulinzi utaimarishwa masaa 24, ili hata wale ambao hawajawahi ona dhahabu wazione na waamini kuwa Geita ni tajiri”, kisha kuwashukuru wawakilishi kutoka TanTrade na Wizara ya Madini katika kufanikisha maandalizi.
Amewaeleza kuwa lengo la Mkoa ni kukuza uchumi wa wachimbaji na wanaojishughulisha na uzalishaji madini ya dhahabu, hivyo umefika wakati majibu sahihi juu ya changamoto zinazowakabili kupatikana na si kwa namna nyingine bali maonesho hayo. Alimaliza kwa kuwashukuru wadau kwa kuchangia ufanikishaji wa shughuli hiyo kwa ahadi za awali zaidi ya Milioni Themanini na fedha taslimu Shilingi Milioni Nne na Laki Tano kutoka kwa wadau zaidi ya sitini.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Herman Matemu akawakaribisha wadau kwenye kikao na kutoa rai kwao kuwa, kutokana na ukweli kuwa Mkoa wa Geita unaongoza kwa kuwa na rasilimali kubwa ya Madini ya Dhahabu hadi kupelekea kuandaa maonesho ya kihistoria ili kuibua fursa zinazopatikana kwenye mnyororo wa thamani wa Madini ya Dhahabu ili kuinua kipato cha mwananchi na kuongeza mapato ya serikali ni vyema wadau hao kushiriki.
kwa upande wake Kaimu Kamishna Msaidizi wa Uchumi na Biashara ya Madini, Bw. Godleader Shoo amepongeza Mhe. Mhandisi Gabriel kwa niaba ya Wizara kwa juhudi za mkoa chini ya uongozi wake kwa kutengeneza historia ya maoensho kuandaliwa na mkoa lenye ubunifu wa hali ya juu na kwamba Mhe. Mkuu wa Mkoa anaenda na spidi ya Mhe. Rais katika kukuza uchumi wa Nchi. Amewaeleza wadau hao umuhimu wa kushiriki maonesho hayo na kwamba yatafanikiwa ikiwa watayabeba na kumsaidia Mkuu wa Mkoa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade) Bi. Twilumba Mlelwa akasoma taarifa ya maandalizi ya shughuli hiyo ambapo ilionesha hadi sasa washiriki wameongezeka na kuwa maonesho yatafanikiwa kwa kiasi kikubwa hivyo kuwahimiza wadau wa sekta hiyo kujitokeza kwani itakuwepo pia kliniki ya biashara ambayo itatibu matatizo yote yanayowakwamisha wafanyabiashara katika kufanikiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mhandisi Chacha Wambura amesema kazi iliyofanyika mpaka sasa ni kubwa na akatumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau kushiriki akifafanua juu ya ukubwa wa tukio hili na kwamba maonesho hayo yataacha alama kubwa ndani ya mkoa na yatatoa nafasi ya kubadilishana teknolojia na kupelekea mabadiliko makubwa kwenye shughuli za uzalishaji madini ya dhahabu hivyo si ya kukosa.
Mwisho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Leonard Bugomola aliendesha zoezi la kuchangia ufanikishaji wa maonesho hayo.
kwa hakika, wadau hao wamemthibitishia Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa wapo pamoja naye na watayabeba maonesho na kuhakikisha hayakwami.
Kikao hicho kilihudhuliwa na viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Wahe. Wakuu wa Wilaya za Geita, Wakurugenzi, Makatibu Tawala Wilaya, Wasanii, Waandishi wa Habari pamoja na wawakilishi wa vyama na jumuia za wachimbaji na wachenjuaji wa madini Mkoani Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa