Katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwezesha uanzishaji wa kamati za ulinzi wa Wanawake na Watoto kwa ngazi zote kwenye Mamlaka za Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Hivyobasi, Kupitia maelekezo ya Wizara na ushirikiano ilionao baina yake na mdau Plan International Mkoa wa Geita wameweza kuikutanisha Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto ngazi ya mkoa kwa siku tatu kwa lengo la kuijengea uwezo kuanzia tarehe 26.03.2019.
Akifungua kikaokazi hicho, Elikana Haruni kwaniaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Geita, ameupongeza Mkoa huu kwa jitihada za kufuata maelekezo ya Wizara na kwamba hadi sasa, vijiji 474 vyote vya Mkoa wa Geita vinazo kamati tayari pamoja na mitaa 65 ndani ya Halmashauri ya Mji Geita.
Amesema, “kama mkoa ni vyema tujipongeze kwa kutekeleza maelekezo ya wizara kwakuwa tumeunda kamati hizi kwa asilimia 100 katika ngazi zote mkoani hapa. Lakini pia niwashukuru Plan International kwa kukubali kuwezesha shughuli hii, lakini niendelee kuomba wadau kujitokeza kuzijengea uwezo kamati ambazo bado hazijafikiwa ili kwa pamoja tuweze kutekeleza kazi hii ya ulinzi wa wanawake na watoto kwa ufanisi”.
kisha Haruni akamaliza kwa kuwaasa wajumbe na jamii kutokaa kimya wanapoona matukio ya ukatili akisema "tusifiche taarifa za ukatili wanaofanyiwa wenzetu kwakuwa tukinyamaza wataendelea kuumizwa"
Christopher Mushi ambaye ni mwezeshaji kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema, wizara imefurahishwa na hatua iliyofikiwa na mkoa kwa kuunda kamati katika ngazi zote, kuahidi kuwa watakuwa tayari kuendelea kutoa ushirikiano kila itakapohitajika.
Awali, Marcely Madubi, Meneja wa Shirika la Plan International Mkoa wa Geita alisema, ni vyema washiriki kuzingatia yote yatakayoelekezwa ili kuonesha matokeo kuliko kutoyafanyia kazi ikiwa ni kurudisha nyuma juhudi ama jitihada mbalimbali ambazo wao kama wadau wamekuwa wakizifanya katika kumlinda mwanamke na mtoto hasa wa kike kama ilivyo kwenye majukumu yao huku akiomba jitihada iongezwe kuzuia mimba za utotoni kama sehemu ya ukatili kwa watoto wa kike.
Kamati hiyo kwa ngazi ya mkoa inajumuisha wajumbe kutoka uwakilishi mbalimbali kutoka Sekretaieti ya Mkoa na Wawakilishi wa Wenye Ulemavu, Watu Maarufu, Taasisi za Kidini, Mabaraza ya Watoto, Vijana, Wadau wa Maendeleo na Wawakilishi wa Sekta binafsi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa