Wadau Waagizwa Kuhamasisha Zoezi la Uboreshaji Daftari
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs C.M. Mwambegele amewaasa wadau mbalimbali wa Uchaguzi katika Mkoa wa Geita kuhakikisha wanashirikiana na Tume kuwahamasisha wananchi wenye sifa ya kujiandikisha kuwa wapiga kura wanajitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura linalotaraji kuanza tarehe 05/8-11/08/2024 katika Mkoa wa Geita.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ametoa kauli hiyo tarehe 24/7/2024 wakati wa kikao cha wadau mbalimbali wa Uchaguzi kujadili maandalizi ya zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa eneo la Magogo Geita mjini.
Mhe. Jaji Mwambegele ameongeza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ina matumaini kuwa wadau waliopata fursa ya kushiriki katika mkutano huo watakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili zoezi lifanyike kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
“Katika kuhakikisha tunaenda sambamba na mabadiliko ya Teknolojia, Tume imerahisisha zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kwa mara ya kwanza mfumo wa uandikishaji utamwezesha mpiga kura aliyepo kwenye Daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia aina zote za simu au kompyuta.” Aliongeza Mhe. Jaji Mwambegele.
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi Ndg. Ramadhani Kailima amesema kuwa Mkoa wa Geita una vituo 1,637 vitakavyotumika katika zoezi la uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 68 katika vituo 1,569 vilivyotumika kwenye uboreshaji wa mwaka 2019/20. Kadhalika Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 299,672 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24.7 ya wapiga kura 1,212,146 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lillizinduliwa tarehe 20 Julai 2024 katika Mkoa wa Kigoma, Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa( MB) ambapo kwa sasa zoezi liko katika mzunguko wa pili wa uboreshaji unaojumuisha Mkoa wa Geita na Kagera.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mwaka 2024/25 linaongozwa na Kauli mbiu isemayo``Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa