Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg. Mohamed Gombati ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo wote katika Mkoa wa Geita kuhakikisha wanajisajili ili kutambulika na kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali katika kuwainua Zaidi kiuchumi.
Ndg. Mohamed Gombati ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na Wataalam kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum waliofika Mkoani Geita kwa lengo la ufuatiliaji wa zoezi la wafanyabiashara wadogo linaloendelea Nchini kote.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita ameeleza kuwa katika Mkoa wa Geita jumla ya wafanyabiashara 142 wameshajisajili na Serikali imeendelea kujenga mazingira wezeshi ya ufanyaji shughuli zao za kibiashara kwa kutoa fursa za mikopo yenye riba nafuu kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za kifedha.
“Ushirikiano baina ya Serikali na wafanyabiashara wadogo utaendelea kuimarishwa ili kuweza kupata matokeo ambayo wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanayategemea.” Aliongeza Ndg. Mohamed Gombati.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Carlos Gwamagobe amesema kuwa Serikali imetoa Zaidi ya Shilingi Bilioni nane kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo kupitia Benki ya NMB hivyo wafanyabiashara wadogo wanatakiwa wasajiliwe ili kukidhi vigezo vya kupata mkopo wenye riba nafuu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wadogo Mkoa wa Geita Ndg. Maulid Said ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafanyabiashara wadogo na kuwapatia fursa ya mikopo yenye riba nafuu na kuahidi kuwa atahakikisha zoezi la usajili katika Mkoa wa Geita linafanikiwa kama ilivyolengwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa