Wafanyakazi wa Taasisi za Umma pamoja na zile za binafsi katika Mkoa wa Geita wamepewa rai ya kuhamasishana ili kila mmoja aboreshe taarifa zake katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la wapiga kura, zoezi ambalo limeanza tarehe Mosi mwezi Mei na kumalizika tarehe 7 Mei 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela ametoa rai hiyo tarehe 01 Mei 2025 alipokuwa akizungumza na hadhara ya watumishi wa Mkoa wa Geita wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika katika viwanja vya CCM Kalangalala Manispaa ya Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amefafanua kuwa wafanyakazi wakiboresha taarifa zao watapata fursa ya kuchagua viongozi ambao wana sera za kuwasaidia wafanyakazi katika changamoto zinazowakabili, pamoja na kuwapima viongozi waliokuwa madarakani awali na wametia nia ya kuendelea jinsi walivyowasaidia watumishi wao walipokuwa madarakani.
Mhe. Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia Mkoa wa Geita fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali zikiwemo Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameeleza kuwa Serikali imeidhinisha kiasi cha shilingi Bilioni 7.7 kwa ajili ya kulipa madai na malimbikizo ya mishahara, likizo na masaa ya ziada kwa watumishi wa Umma Mkoani Geita kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Kadhalika Mkuu wa Mkoa wa Geita ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuridhia kutoa fedha hiyo ili kuondoa malalamiko na kutengeneza mazingira rafiki ya wafanyakazi wakiwa Ofisini na nje ya ofisi. Pamoja na kuupatia Mkoa wa Geita watumishi wapya 8,424 kati yao 6,202 wakiwa ni walimu.
Maadhimisho ya Mei Mosi yalikwenda sambamba na tukio la Mkoa wa Geita kugawa pikipiki 20 kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa mzima ikiwa ni jitihada za Serikali katika kuwarahisishia utendaji kazi Maafisa hao. Pikipiki hizo zimenunuliwa kwa gharama ya shilingi Milioni 75,306,000
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wote, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Geita Ndg. Magilu Ndebile Kabengwe ametoa ombi kwa Serikali kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi ikiwa ni pamoja na baadhi ya waajiri kusuasua kuwasilisha michango ya watumishi hasa wa Sekta binafsi, ucheleweshaji wa malipo ya likizo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara nk.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakumbuka na kutambua jitihada zilizofanywa na wafanyakazi walioandamana kupigania haki za wafanyakazi Duniani, kwa mwaka 2025 Maadhimisho hayo yaliongozwa na Kauli Mbiu isemayo “ Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa