Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela amewaapisha rasmi wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Bukombe.
Akizungumza wakati wa zoezi la uapisho wa wajumbe hao lililofanyika tarehe 8/7/2014 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita eneo la Magogo Geita mjini, Mhe. Shigela amewapongeza wajumbe hao kwa heshima kubwa waliyoipata ya kuwa watu waliounda Baraza la kwanza la Ardhi katika Wilaya ya Bukombe na kuwasihi kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria zinazowaongoza.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa uwepo wa Baraza hilo uhakikishe unaenda kuanza kazi mara moja ili changamoto zilizopo kuhusiana na masuala ya ardhi katika jamii ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka na ana imani kuwa wajumbe hao watakuwa ni chachu katika kwenda kutatua changamoto za masuala ya Ardhi zilizopo katika jamii yao.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndugu. Mohamed Gombati amewashauri wajumbe wa Baraza hilo Kuyafanyia kazi maneno matatu waliyoyatamka katika kiapo chao ambayo ni kuzingatia wanakuwa waaminifu katika utendaji kazi wa kila siku,kuwa waadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya kupokea rushwa pamoja na kumuomba Mungu kila wanapotimiza majukumu yao ili awaongoze katika shughuli zao .
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya la Geita Ndugu Asha Maganya amewaeleza wajumbe hao kutambua kuwa wao ni watu wa muhimu sana ambao wapo kwa mujibu wa sheria na taratibu kwa ajili ya kusimamia haki za watu katika jamii yao, hivyo wanatakiwa wakafanye kazi kwa bidii ili kuendelea kujenga imani na uaminifu kwa Waziri mwenye dhamana ambaye ameridhia wao kuwa wajumbe watakaotatua migogoro ya Ardhi katika Wilaya ya Bukombe.
Ndg. Asha Maganya amewaasa wajumbe hao kuwa wasiri katika uendeshaji wa shughuli za Baraza, kujiepusha na tabia za kutokuwa madalali katika kusimamia haki za watu kwa kuepukana kabisa na vitendo vya kupokea rushwa pamoja na upendeleo wa aina yeyote. Kadhalika ametoa pendekezo kwa Wakurugenzi wote katika Halmashauri za Mkoa wa Geita kuandaa kikao kazi na wajumbe wa mabaraza ya kata ili kuwajengea uwezo kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wao.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wajumbe wenzake walioteuliwa Bi. Bianchi Nasibu Mwebeyo ametoa shukrani za dhati kwa viongozi wa Serikali walioshiriki kwa namna moja hadi nyingine kuwachagua wao miongoni mwa wengi, ameahidi kufanya kazi kwa misingi ya sheria Ardhi na Nyumba huku wakitegemea kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla.
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Bukombe linaundwa na wajumbe wanne ambao ni Ndugu. Kevin Stephen Makonda, Bi. Bianchi Nasibu Mwebeyo , Ndugu. Bukiga Bandeke Stanslaus na Bi. Jalia Mkubila Sudi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa