Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela amewaagiza wakandarasi watakaotekeleza kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara katika Wilaya zote za mkoa wa Geita kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kuhakikisha wanatimiza falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha kazi wakati na ubora uliokubalika.
Mhe. Shigela ametoa kauli hiyo tarehe 5/08/2024 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita eneo la Magogo alipokuwa akizungumza na wakandarasi wazawa pamoja na wataalam wa Wakala wa Barabara za vijijini na mijini( TARURA) wakati wa hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba kati ya TARURA na Wakandarasi watakaotekeleza shughuli hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa mikataba ikamilishwe ndani ya kipindi cha miezi sita ili kumaliza ujenzi kwa wakati kabla ya msimu wa mvua kuanza sambamba na kutiliwa mkazo kwa kipengele cha ubora wa barabara hizo ili wananchi waweze kunufaika na wakandarasi wenyewe kujiwekea rekodi nzuri ya kampuni zao kukumbukwa katika kazi nyingine.
“Napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya kuhakikisha watanzania wote wakiwemo wa Mkoa wa Geita wanapata miundombinu bora ya barabara itakayowarahisishia shughuli zote za usafiri na usafirishaji pamoja na fursa nyingine zitakazopatikana wakati wa matengenezo ya barabara hizo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wetu.” Aliongeza Mhe. Shigela.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Geita Mhandisi David J. Msechu amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya shilingi 20,239,286,847.55 kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Mfuko wa barabara( Road fund), Mfuko wa jimbo, Mfuko wa Tozo za Mafuta na Mfuko wa Maendeleo barabara zimeidhinishwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi, ukrabati na matengenezo ya barabara katika Mkoa wa Geita.
Mhandisi David Msechu ameongeza kuwa wataalam wote wa TARURA wamejipanga kusimamia kikamilifu na kwa weledi mkubwa utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuweza kumalizika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kuboreshewa huduma za usafiri na usafirishaji, kuwezesha huduma za jamii kama elimu na afya kupatikana kiurahisi, kuongeza ajira kwa wananchi walioko katika maeneo ya kazi na kuinua uchumi pamoja na kuondoa umaskini kwa jamii.
Mikataba 24 yenye jumla ya thamani ya Shilingi Bilioni 9.608 imesainiwa na inategemewa kuanza baada ya siku 14 na itatekelezwa kwa muda wa miezi sita kwenye wilaya zote ndani ya Mkoa wa Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa