Wakurugenzi Geita watakiwa kutenga Fedha za Vikundi vya Akina Mama, Vijana na Walemavu
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mkoani Geita kutenga fedha ili kuviwezesha vikundi vya akina mama(Asilimia 4), Vijana(Asilimia 4) na wenye Ulemavu (Asilimia 2) kujikwamua kiuchumi.
Akihutubia wananchi wa Wilaya ya Bukombe katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Mheshimiwa Robert Gabriel amesema kuwa dira ya Serikali ya awamu ya tano iliyo chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa Viwanda hivyo wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika harakati za kuchochea ukuaji wa uchumi ndani ya nchi kupitia vikundi vya kiuchumi, VICOBA, SACCOS na vikundi vya kijamii. Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa wanawake wamekuwa wakijihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile uchakataji wa malighafi ili kuongeza thamani, biashara ndogondogo, ufugaji, ushonaji, kilimo cha mazao na bustani za mboga na matunda ili kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa kaya na kutoa mchango katika uchumi wa taifa kupitia sekta isiyo rasmi.
Aidha, amezitaka Halmashauri kuendelea kuchambua na kuvitambua vikundi vya Wanawake na Vijana vyenye mwelekeo wa Viwanda na kuzalisha malighafi kwa ajili ya kulisha viwanda vidogo na vya kati ili vijengewe uwezo kifedha, mafunzo na vifaa ili vichangie azma ya Serikali.
Vile vile Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa ufike wakati jamii ione umuhimu wa kuwalinda Wanawake na Wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili kimwili kama vipigo, ubakwaji, ndoa za utotoni na kuwarubuni kimapenzi mabinti wadogo kwa kuwa vitendo hivi vinachangia kwa kiasi kikubwa kukatisha ndoto zao za kujiendeleza kiuchumi, hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya kaya na taifa.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Geita yamefanyika Wilayani Bukombe kwa kauli mbiu ya ''Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake Vijijini''.Ambapo Wanawake wajitokeza kuonyesha bidhaa na shughuli zao mbalimbali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa