WAKUU WA MIKOA, WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI WATAKIWA KUSIMAMIA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA HALMASHAURI
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wametakiwa kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali pamoja na wafadhili ili zifanye kazi ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika mamlaka za Serikali za mitaa.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chato katika hafla ya kukabidhi nyumba 50 na kiwanda cha kukamua alizeti Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa katika Halmashauri kumekuwa na upotevu mkubwa na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma mbalimbali kwa wananchi."Bajeti ya dawa imeongezwa kutoka bilioni 31 hadi bilioni 250 natoa wito kwa wakuu wa mikoa,Wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kusimamia matumizi ya fedha kwa kuwa katika Halmashauri nyingi fedha zimekuwa zikitumika vibaya hivyo msimamie".Amesema fedha za pembejeo na mfuko wa barabara zimekuwa zikitumika vibaya hivyo viongozi wote wasimamie miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, katika mkutano huo Mheshimiwa Rais ameseme kuwa leseni za madini zisitolewe tena kwa wawekezaji mpaka pale serikali itakapojipanga vizuri. Katika hafla hiyo mheshimiwa Benjamini Mkapa amekabidhi nyumba 50 zilizojengwa na Taasisi ya Benjamini Mkapa katika Mikoa ya Geita (20),Kagera910) na Simiyu(20) kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5.
Katika hatua nyingine Balozi wa Japan nchini amekabidhi kiwanda cha kukamua alizeti chenye uwezo wa kukamua lita 700 kwa siku kilichojengwa na Serikali ya Japan Chato mjini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa