Zaidi ya wanahabari 20 wamepata fursa kushiriki mafunzo kuhusu Utekelezaji wa Mradi wa utoaji huduma za Tohara kinga kwa wanaume kama Afua mojawapo ya kuzuia maambukizi ya VVU katika mkoa wa Geita, mradi wa miaka mitano kuanzia mwaka (2016-2021),
Hayo yamedhihirika wakati wa mafunzo kwa waandishi wa Habari wa mikoa ya kanda ya ziwa yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Alphendo uliopo Mjini Geita.
Akifungua mafunzo hayo yalioandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la IntraHealth International Inc, kwa ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) PEPFAR kupitia CDC, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Japhet Simeo amewataka waandishi kusaidia ufikishaji wa taarifa sahihi kwa wananchi na kwa wakati.
“Tunaamini kuwa nyie ni chachu ya kufikisha taarifa, lakini leo tumewaita hapa lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha mnatusaidia kufikisha habari hii mahali ambapo hatufiki, mkizifikisha kwa usahihi na tutawapitisha kujua hali halisi ya maambukizi na mjue mbinu gani tunazotumia” amesema Dkt. Simeo.
Dkt. Simeo ameendelea kusema kuwa, wanahabari ni muhimu kukumbuka juu ya sheria zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Huduma za Habari na ya Takwimu ambapo ni wajibu wa kila mtoa habari au taarifa kutoa takwimu zilizo sahihi, sizizowachanganya wananchi, zinazochochea maendeleo na si migogoro huku wananchi wakipata haki yao ya kupata taarifa,
Vilevile ameeleza changamoto ya kutoweza kuwabakisha wananchi waliogundulika kuwa na maambukizi ya UKIMWI ili waendelee kupata dawa za kufubaza maambukizi hayo kutokana na aina ya shughuli za kiuchumi wanazojiusisha nazo mkoani Geita kama vile ufugaji, uvuvi na uchimbaji madini, shughuli zinazosababisha uhamaji wa wananchi hawa.
Aidha Dkt. Simeo alieleza kuwa zipo jitihada kuhakikisha maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutokana na ongezeko lililopo kwa sasa kutoka asilimia 4.7% hadi 5% ambalo limetokana na uwepo kampeni zinazoendelea kufanyika juu ya tohara huku ikihakikishwa wote wanaofanyiwa tohara wanapimwa na VVU.
Akitambulisha Shirika la IntraHealth International Inc, Dkt. Peter Sewa ambaye ni Mshauri Huduma za Tohara Mkoa wa Geita alisema wanatarajia kuanza kufanya tohara kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia mwaka 0 hadi miezi 2 kwa mwaka 2019
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Temigunga Mahondo amewataka waandishi kuzingatia weledi katika uhabarishaji wa sekta ya afya wakitambua kuwa wao ni wafikisha taarifa kwa jamii na kwamba endapo watapotosha wataharibu sifa yao binafsi lakini pia jina la chombo wanachokitumikia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa