Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amewataka wananchi wa mkoa huo kuwa na utaratibu wa kutunza vyanzo vya maji ambavyo vimekuwa ni muhimu kwao.
Ameyasema hayo leo Mei 31, 2022 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji mradi wa kuboresha huduma ya maji mjini Geita unaotekelezwa na serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA).
"naipongeza GEUWASA kwa kazi kubwa wanayoifanya, jambo hili limenilidhisha kuona mradi huo unakamilika hata kabla ya wakati uliopangwa" amesema Mh. Senyamule
Amesema pia wananchi zaidi ya 6,250 watanufaika na mradi huu, hivyo ameutaka Uongozi kuhakikisha kukamilika kwa mradi huo kama yalivyo maelekezo ya serikali ili wananchi wapate huduma kwa wakati.
Ikiwa zimebakia siku 30 kufikia tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, Mh. Senyamule alisema,
“tunamshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwakuwa yeye alikuwa na utashi wa kupambana na janga la UVIKO kwa kuamua kutoa fedha hizo kujenga miradi mbalimbali ikiwemo huu wa maji ambao utachangia ongezeko la 4% na kuufanya mji wa Geita kupata maji kwa 75% kutoka 71% ya awali na kuwezesha wananchi takribani 6,250 kupata huduma ya maji. Vilevile, niwapongeze GEUWASA kwa utekelezaji unaozingatia muda na hivyo niagize na taasisi nyingine zenye ujenzi wa miundombinu kwa fedha za mapambano dhidi ya UVIKO-19 kukamilisha miradi hiyo mapema iwezekanavyo”.
Mhe.Senyamule aliongeza kuwa, ni vyema GEUWASA kuhakikisha wanapanda miti rafiki kwa mazingira ili kuendelea kutunza vyanzo vya maji lakini pia kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wasiharibu vyanzo hivyo na kutoa wito kwa wananchi kutumia vizuri rasiliamali maji na kuwa walinzi wa miundombinu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka juu ya uharibifu au wizi wa miundombinu hiyo.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji mradi, mhandisi Isaac Mgeni alisema, mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Tshs.511,906,928.22, unalenga kuwahudumia wananchi wa Ishinde, Igembesabho, Fadhili Bucha, Mwabasabi, Kasamwa, Kanyala na Buhalahala pale utakapokamilika kwakuwa hadi sasa upo kwenye 98% ya utekelezaji na kwamba hadi sasa, jumla ya wateja wapya 123 wa maeneo ya Kasamwa na Buhalahala wamekwisha unganishiwa huduma hiyo.
Naye Ndg.Nestory Madaha kwaniaba ya Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kasamwa kinachohudumia takribani wateja 1,500-2,000 alisema, “tunaishukuru sana serikali yetu pendwa kwa kutueletea huduma ya maji ambapo awali tulitumia fedha nyingi kununua maji na kwa hatua hii, kituo chetu kitaendelea kuwa kisafi, wagonjwa wanapata huduma nzuri na tutaepuka magonjwa yatikanayo na uchafu”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa