Ni tarehe 12.03.2019, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb) anawasili katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita na kueleza lengo la ziara yake mkoani hapa.
Mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Mhandisi Robert Gabriel anampokea, kisha Mhe. Dkt. Mabula anapata fursa ya kuelezea juu ya ujio wake.
Na hapa Mhe. Dkt. Mabula anasema, “nashukuru kwa mapokezi, lakini leo nitakwenda katika Miji ya Katoro Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Buseresere katika Halmashari ya Wilaya ya Chato kwa lengo la kugawa hati kama kichocheo kuwahamasisha na wengine ambao bado hawajalipia kupimiwa wafanye hivyo. Tungependa miji hii ikue katika mpangilio, iwe na mwonekano mzuri, na ni vizuri tukiyawahi yale maeneo ambayo hajaharibika ili tusirudie makosa ya awali. Watumishi wa ardhi wa Geita Vijijini sasa ni muhimu kuhamia maeneo haya yanayokuwa ikiwemo katoro ili kumrahisishia mwananchi ulipaji, lakini pia itasaidia upangaji mzuri kwakuwa unapokuwa mbali na wananchi huwezi kufanikisha zoezi la utoaji hati na viwanja ”
Vile vile Mhe. Naibu Waziri ameonesha kutoridhishwa na idadi ndogo ya umilikishaji hati kwa wananchi kwakuwa Mkoa umemilikisha hati mia moja (100) pekee hadi sasa. Ukiacha hilo, bado ukusanyaji wa madhuhuri ya serikali ni mdogo kufuatia takwimu katika taarifa ya mkoa iliyosomwa na mtaalam wa ardhi iliiyo onesha kuwa, hadi sasa Mkoa huu umekusanya jumla ya Tshs. Milioni 152.6 kati ya lengo la Tshs Bil Moja na zaidi na kwamba tayari tumevuka nusu mwaka hivyo haoni kama kuna dalili za kufikiwa kwa malengo.
Dkt. Mabula akawakumbusha wataalam wa ardhi kuzingatia maagizo ikiwa ni katika kipindi kifupi alipozulu mkoani hapa na kutoa maagizo ikiwemo ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa wale ambao bado hawajalipa fedha wanazodaiwa baada ya kupata taarifa kuwa hakuna hata mmoja aliyepelekwa mahakamani.
Pamoja na hayo, bado imeelekezwa kuwa, ni vyema TARURA kupitisha barabara kwenye maeneo yaliyorasimishwa ili wananchi waone kweli serikali imeamua kurasimisha maeneo hayo kutokana na kwamba uzoefu unaonesha kuwa, maeneo yaliyorasimishwa bila kuwekewa miundombinu katika ile mipango iliyokubalika na jamii, ni vigumu wananchi kuanza kuyaendeleza.
Akimaliza kusema ,Dkt. Mabula ameendelea kuzisihi Halmashauri kuazima vifaa kwenye ofisi za ardhi za kanda ili kazi isikwame, vifaa ambavyo haviitaji kulipiwa, na pia kumwomba Mkuu wa Mkoa kuwafuatilia kwa karibu wataalam wa ardhi na halmashauri kwa ujumla, kuangalia uwezekano wa mabadiliko ya watumishi ndani kwa ndani ili kuboresha na pengine kutumia ufanyaji kazi wa timu kwa kuazima wataalamu wa halmashauri nyingine kisha kuendelea na ziara yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameonesha kutoridhishwa na namna watumishi wa ardhi wanavyotekeleza maagizo akisema “ kwa taarifa hizi tulizozisikia juu ya upimaji , urasimishaji , umikishaji na utoaji hati, inaonesha dhahiri kuwa huenda watumishi wa ardhi hatuwajibiki, hatujui majukumu yetu, hatuna utaalamu, au hatuna mpango kazi na pengine huenda tumeweka gharama kubwa. Niwaambie kuwa, umaskini pia unachangiwa na ukaaji holela kwenye miji”.
Kufuatia maelekezo ya Naibu Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Geita akaelekeza kuwepo kwa kikao ndani ya wiki moja, na wataalam wa ardhi kuleta taarifa kwa kamati ya usalama mkoa, wakieleza changamoto ni ipi na kuwashauri kupata uzoefu kwa waliofanya vizuri, huku akimhaidi Naibu Waziri kuwafuatilia sekta ya ardhi ndani ya mkoa kuhakikisha yote yaliyosemwa yanatekelezwa kurekebisha taarifa hiyo ambayo si nzuri kwa mkoa huu. Mwisho, Mhandisi Gabriel akamkaribisha Mhe.Dkt.Mabula kushiriki ufunguzi wa soko la madini ya dhahabu Geita utakaofanyika tarehe 14.03.2019.
Awali akisoma taarifa kwa Mhe. Naibu Waziri, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Bw. Huzuria Kyungu amesema, kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2019, jumla ya viwanja 704 vimepimwa, jumla ya hati miliki 586 zimetolewa na mazoezi ya uhamasishaji yanaendelea hasa kwa yale maeneo yaliyofanyiwa urasimishaji wa makazi holela.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Elisha Lupuga akatumia fursa hiyo kumwomba Mhe. Naibu Waziri kuongezewa idadi ya watumishi kwakuwa halmashauri anayoisimamia ina eneo kubwa la kiutawala na kwamba watatekeleza maagizo yake ikiwemo la kuwahamishia wataalamu Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro ili kusogeza huduma kwa jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa