Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi Milioni 50 kwa Taasisi ya Wanawake na Samia wa Mkoa wa Geita kwa ajili ya kuongeza mtaji wa zabuni ya kuwalisha watumishi Zaidi ya mia moja kwa siku wa Shirika la Madini la Taifa( STAMICO) ambao wanafanya kazi ndani ya mgodi wa GGM.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutembelea banda la wanawake na Samia wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya saba ya Teknolojia ya Madini Geita kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo na kuguswa na kazi wanazozifanya ikiwemo zabuni ya utoaji chakula na kuvutiwa na jitihada zinazofanywa na wanawake hao.
Akiwakabidhi risiti ya fedha hizo tarehe 21/10/2024 Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amewaasa wanawake hao kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukuza mtaji na kupanua wigo wa kutoa huduma ya chakula katika makampuni mengine na kuwa chachu ya kupiga hatua Zaidi na kuwainua kiuchumi.
“Fedha mliyopewa siyo ya kwenda kugawana posho wala nauli bali iwasaidie kuinua mtaji utakaotengeneza faida ambayo itawezesha Taasisi ya Wanawake na Samia kuimarika Zaidi kimkoa na hata kitaifa.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Ndg. Adelina Lambert Kabakama ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaongezea mtaji utakaowainua Zaidi na kuwafanya wasikope kwenye taasisi nyingine za kifedha.
Ndg. Adelina Kabakama kadhalika amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Geita pamoja na ofisi yake kwa kuwa nao bega kwa bega siku zote katika kuwashauri na kuwaongoza. Pia amewahamasisha wanawake na Samia katika wilaya zote za Mkoa wa Geita kubuni biashara za aina mbalimbali katika maeneo yao.
Taasisi ya Wanawake na Samia pia ni mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes unaozalishwa na STAMICO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa