Wanawake waishio katika Halmashauri zote za Mkoa wa Geita wamesisitizwa kuhakikisha wanajiunga na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya vijiji na mitaa ili waweze kutambulika na kuunganishwa kwenye fursa mbalimbali zinazopatikana ambazo zitawawezesha kujikwamua kimaisha wao binafsi pamoja na familia zao.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum Ndg. Felister Mdemu alipofanya ziara ya kikazi katika Halmashauri za Mji Geita, Wilaya ya Geita na Bukombe kwa lengo la kuzungumza na makundi ya wanawake yanayoratibiwa na Wizara yake pamoja na kukagua shughuli zao wanazozifanya.
Ndg. Felister Mdemu ametoa pongezi kwa Mkoa wa Geita kwa kufikisha wanachama 11765 ambao wameshajiunga na Jukwaa la Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi katika Halmashauri zote za mkoa wa Geita kwa lengo la kuwawezesha wanawake hao kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo yao.
“Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii wote wa Mkoa wa Geita kwa namna mnavyofanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano mkubwa, hakika jitihada zenu zimejidhihirisha. Pia natoa wito kwa jamii, Taasisi za Serikali na watu binafsi katika Mkoa wa Geita kuunga mkono juhudi za wanawake kwa kununua bidhaa wanazozalisha kwa wingi hususan wakati wa sherehe na matukio mbalimbali ambapo bidhaa hizo zitahitajika.” Aliongeza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya jinsia katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Juliana Kibonde ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa kuanzisha vikundi 12 ambavyo vimezaliwa kutoka katika Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe na kushauri Halmashauri nyingine za Mkoa wa Geita kuiga mfano huo ili wanawake wengi Zaidi waliopo kwenye jamii waweze kujiunga na vikundi ili wawezeshwe kiuchumi na kukataa kabisa ukatili wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Geita Bi. Wancy Siwale ameeleza baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa na jukwaa hilo ni pamoja na kuanzisha SACCOS, kushiriki katika shughuli mbalimbali za jukwaa kitaifa kama Kampeni ya 27 ya kijani pamoja na kuendelea kushirikiana na Taasisi za Serikali, binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika jitihada za kuwakwamua wanawake kiuchumi.
Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 na uwepo wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ni utekelezaji wa progamu ya kitaifa ya Jukwaa la kizazi chenye usawa ambalo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara katika utekelezaji wa eneo namba 2 la Haki na Usawa kiuchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa