Serikali imewataka Maafisa Habari wa mikoa na halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu jukumu lao la kuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikali katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa wakati wa akifunga kikao kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Mtumba jijini Dodoma.
Amesisitiza kuwa wananchi wanahitaji taarifa sahihi, kwa wakati, na zenye kueleweka kuhusu miradi ya maendeleo, huduma za kijamii, na mikakati ya serikali ya kuwahudumia.
"Maafisa Habari mnapaswa kuwa sauti ya serikali katika maeneo yenu. Mna wajibu wa kuhakikisha mafanikio ya serikali yanawafikia wananchi, na pia changamoto zinazojitokeza zinaelezwa kwa uhalisia wake," aliongeza Msigwa.
Katibu Mkuu ameeleza kuwa kutofikisha taarifa kwa wananchi kunapunguza uelewa na ushiriki wao katika utekelezaji wa sera na mipango ya serikali, jambo ambalo linaweza kusababisha upotoshaji au malalamiko yasiyo na msingi.
Serikali imeahidi kuendelea kuwawezesha maafisa habari kwa kuwapatia mafunzo, vifaa na teknolojia ya kisasa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Vilevile, amewahimiza maafisa habari kushirikiana na vyombo vya habari vya kitaifa na vya jamii katika kueneza taarifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa