Wataalam wa sekta ya ardhi mkoani geita wakiwemo maafisa ardhi, maafisa mipango miji, wapima ardhi, warasimu ramani na wathamini wameendelea kukutana ili kujiimarisha katika utendaji kazi wao huku wakihimizwa kuwa waadilifu ili kuepuka migogoro ya ardhi, ikiwa ni miezi saba tangu kukutana na waziri mwenye dhamana na ardhi mhe Lukuvi wakati wa ufunguzi wa ofisi za ardhi mkoa, kikao kilichofanyika oktoba 16, 2020 kwenye ukumbi wa mikutano, ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita.
Akifungua kikao cha wataalam hao, mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel alisema, ni muhimu watumishi wa ardhi kufanya kazi kwa uadilifua na uaminifu, jambo litakalomaliza migogoro ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi wengi ambao walihangaika sana kwa wingi wa migogoro ambayo mingine ilisababishwa na watalaam, hivyo wanapaswa kuisaidia serikali kwenye eneo hilo.
"sekta hii ni sehemu iliyoumiza wengi, na wananchi waliitafsiri ardhi kama kitu kinachoweza kumilikiwa kwa utaratibu na matajiri tu kwani wengi walizungushwa sana hata katika upatikanaji wa hati na wengine kunyang'anywa viwanja vyao na wenye nguvu ya fedha, hivyo ninyi isaidieni serikali kwa kufanya kazi zenu kwa uadilifu na uaminifu", alisema mhandisi gabriel.
Alisema, anaishukuru ofisi ya kamishna wa ardhi mkoa kwa kuendelea kuusaidia mkoa katika kupunguza changamoto na migogoro ya ardhi ambayo imekuwepo mkoani geita kwa kipindi kirefu, huku akihimiza wataalam hao kuendelea kutoa elimu ya ardhi kwa wananchi na kwamba ni uchumi ikiwa watajua thamani yake, lakini vilevile kuendelea kupima ardhi kwa gharama nafuu, kupanga miji na kuzisaidia halmashauri zao kuwa na mipango bora ya matumizi ardhi.
Naye kamishna msaidizi wa ardhi mkoa wa geita ndg.Rugambwa Banyikila alimshukuru mhandisi Gabriel kutokana na matunda ya kazi anazozisimamia ikiwemo kutoa dira ya mhe Rais kwenye eneo la ardhi na kwamba wao kama wataalam wataendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuleta maendeleo kwa pamoja na kupunguza hatimaye kuondoa migogoro yote ya ardhi.
kikao hicho kilihudhuriwa na wataalam hao wa ardhi kutoka wilaya zote za mkoa wa geita yani geita, chato, bukombe, mbogwe na nyang'hwale.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa