Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Denis Bandisa amewataka watumishi wa Umma ndani ya Mkoa wa Geita kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano na kwamba habaki nyuma hata mtumishi mmoja, lengo ikiwa ni kufikisha huduma zilizo bora kwa wananchi. Bw. Bandisa ameyasema hayo alipoitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale tarehe 03.09.2018 na kuongea na watumishi wa Halmashauri hiyo katika ukumbi wa wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Bw. Bandisa ameanza kwa kuwaambia watumishi hao kuwa, amewatembelea ili kujitambulisha kwao, lakini pia kuwakumbusha misingi ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo la ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya watumishi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) zilizowekwa.
Amesema, “pamoja na kujitambulisha, nawakumbusha juu ya ukusanyaji wa mapato, kwani hili si jukumu la mtu mmoja, bali watumishi wote. Hakikisheni mnaongeza mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, lakini pia kwakuwa tupo kwenye kipindi cha mtihani wa darasa la saba, hakikisheni mnakuwa sehemu ya kufanikisha kufanyika vyema kwa mtihani huu kwa kuwa walinzi wa kufichua wale wote wenye kutaka kuharibu zoezi hili muhimu la kitaifa".
Pia amewakumbusha watumishi kuepuka kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi akiwataka Maafisa Ardhi kuwajibika na Maafisa Mazingira kusimamia vyema sheria za mazingira hasa kwa wachimbaji ambao wengi wao wamekuwa wakikiuka sheria kwa kuanza shughuli za uchimbaji pasipo kuwaondoa kwa fidia wakazi wanaoishi maeneo husika jambo ambalo linalopelekea kuwa na migogoro mingi.
Nidhamu kwa watumishi, imekuwa ni moja ya mada aliyoizungumzia kwa watumishi hao akisisitiza juu ya nidhamu ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ambapo amasema ni lazima fedha zinapoletwa na maelekezo yake yazingatiwe, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakao husika. Kuwa na juhudi kazini, kuwa nadhifu, kuwa tayari kupokea maagizo na maelekezo lakini pia mashirikiano baina yao yalikua ni sehemu ya maelekezo yake kwa watumishi wa mkoa kupitia watumishi wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali Watu Bw. Herman Matemu, amewakumbusha watumishi hao juu ya nidhamu kama kipaumbele lakini pia kufuata taratibu za kiutumishi kuanzia kuwahi kazini na wakuu wa idara na vitengo kuhakikisha wanawasimamia na kuwawajibisha wanaowaongoza akitolea mfano wa idara za elimu na afya akionya watumishi kutofanya shughuli binafsi wakati wa masaa ya kazi.
Katibu Tawala Msaidizi Upande wa Serikali za Mitaa Bi. Sania Mwangakala yeye amehimiza juu ya ufanyaji wa kazi kwa kushirikiana (team work) wakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili mwisho wa siku waweze kutoa huduma bora kwa wananchi. Amekumbusha juu ya kufanya vikao vya kila mwisho wa mwezi jambo linaloweza kuwasaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang’hwale Bi. Mariam Chaulembo kwa niaba ya watumishi alimhaidi Katibu Tawala wa Mkoa kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa na kumshukuru kuwatembelea watumishi hao.
Mwisho, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Fabian Yinza aliwasihi watumishi kupenda kutafuta ushauri pale mambo yanapowawia ugumu kuliko kukaa kimya na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza kwa kuwa lengo kuu ni kufikisha huduma bora kwa wananchi na kwa njia hiyo malalamiko ya wananchi yatapungua, kisha akahairisha kikao hicho.
Awali, kabla ya kuongea na watumishi, Katibu Tawala wa Mkoa na Wataalam wa Sekretarieti ya Mkoa alioambatana nao walipokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Hamim Gwiyama kisha kutembelea na kujionea ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo ulio katika hatua ya msingi inayowashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Geita: “Amani Umoja na Kazi”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa